WAZIRI KIJAJI AIAGIZA TANAPA KUKAMILISHA MIRADI YA MAENDELEO HIFADHI YA TAIFA RUAHA

 

Na. Philipo Hassan – Ruaha

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ameiagiza TANAPA kukamilisha miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha ili miradi hiyo ianze kutumika kwa lengo la kukuza utalii katika ukanda wa kusini mwa Tanzania. 

Waziri Kijaji ameyasema hayo leo Desemba 18, 2025 akiwa katika ziara ya kikazi ndani ya hifadhi hiyo ambapo alifanya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kiganga, Kituo cha kutolea maelezo kwa watalii (VIC), Nyumba za kulala watalii (Cottages) na Kituo cha ufuatiliaji wa kiikolojia, miradi iliyojengwa chini ya mradi wa REGROW.

“Hakikisheni miradi hii inakamilika kwa wakati kama makubaliano na wakandarasi yanavyoelekeza ili sasa utalii wa kusini uweze kufunguka na kuvutia watalii wengi kutembelea hifadhi hatimaye kufikia malengo ya Serikali ya kufikisha watalii Milioni 8 ifikapo mwaka 2030” ~ alisema Mhe. Dkt. Kijaji.

Naye, Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, CPA Musa Nassoro Kuji alieleza kuwa Hifadhi ya Taifa Ruaha inaendelea kubuni mazao mapya ya utalii na kuvutia wawekezaji ili kuitangaza hifadhi hiyo ili kuongeza idadi ya watalii na mapato ndani ya hifadhi na Shirika kwa ujumla.

“Mhe. Waziri, Hifadhi ya Taifa Ruaha tuna mpango wa kuanzisha mazao mapya ya utalii kama utalii wa kuendesha farasi (Horse Riding), utalii wa Chemichemi ya maji moto (HotSpring SPA) na utalii wa kutazama nguzo asili (Natural Pillars). Hivyo basi, kukamilika kwa miradi ya maendeleo, uanzishaji wa mazao mapya ya utalii pamoja na wawekezaji walioonesha nia ya kuwekeza hifadhini utaifanya hifadhi kuongeza idadi kubwa ya watalii na mapato”, alifafanua Kamishna Kuji.

Ziara ya Waziri Dkt. Kijaji ni mwendelezo wa ziara za kikazi ambapo aliambatana na viongozi mbalimbali wa Wizara ikiwa ni pamoja na Mhe. Hamad Chande (Mb) Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Nkoba Mabula Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Thereza Mugobi Mkurugenzi wa Utalii na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Wanyamapori Dkt. Fortunata Msoffe.        

Post a Comment

Previous Post Next Post