Vijana kutoka vijiji vya Ntemba na Kate, wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, wamepongeza juhudi za Serikali katika kuendeleza sekta ya kilimo kupitia mpango wa ruzuku ya mbolea na mbegu.
Akizungumza wakati wa kampeni ya “Mali Shambani: Silaha Mbolea” inayoendeshwa na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), kijana mkulima wa mahindi, Shadrack Maganga amesema mpango wa ruzuku ya pembejeo umebadilisha mtazamo wake kuhusu kilimo na sasa anakiona kama ajira rasmi na fursa ya kiuchumi.
“Naishukuru Serikali kwa mpango wa mbolea ya ruzuku na mbegu kwani zimeniwezesha kuona fursa kwenye kilimo. Nilipoanza nilikuwa ninalima kwa mazoea, lakini sasa ninalima kitaalamu kwani. Katika ekari moja napata kati ya gunia 30 hadi 35 za mahindi, na kwa sasa ninalima ekari 70 na kuvuna takribani gunia 2,000,” alisema Maganga.
Ameongeza kuwa kuelekea msimu wa kilimo wa mwaka 2025/2026, vijana wanapaswa kujitokeza kwa wingi kwenye kilimo kwani Serikali imepunguza gharama za uzalishaji na kuweka mazingira bora ya uzalishaji wa mazao. “Natoa wito kwa vijana wenzangu kuwa fursa ipo kwenye kilimo. Serikali kupitia ruzuku za mbolea imewezesha upatikanaji wa pembejeo kwa urahisi na bei nafuu.
Kwa upande wake, Aron Julius, kijana mkulima kutoka kijiji cha Kate, alisema mpango wa ruzuku umemsaidia kuongeza uzalishaji maradufu katika shamba lake la mahindi. “Kabla ya ruzuku, nilikuwa napata gunia 5 hadi 8 kwa ekari, lakini sasa napata kati ya gunia 25 hadi 30. Ruzuku imenisaidia kwa sababu mbolea napata kwa wakati na kwa bei nafuu. Uzalishaji umeongezeka kwa kiwango kikubwa,” alisema Aron.
Naye Afisa Kilimo wa Wilaya ya Nkasi Emanuel Gamasa amesema kuwa upatikanaji wa mbolea kwa wakati umechangia ongezeko la matumizi na uzalishaji wilayani humo.
Alibainisha kuwa matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka tani 1,700 mwaka 2021/2022 hadi tani 6,000 mwaka 2023/2024, huku uzalishaji wa mazao ukipanda kutoka tani 400,000 hadi tani 600,000 katika kipindi hicho.







