Dkt. Ladislaus Chan’ga, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, akiwasilisha utabiri wa msimu wa kipindi cha Novemba 2025 hadi Aprili 2026, mapema leo Oktoba 17, 2025, jijini Dar es Salaam.
NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa mvua za Msimu kwa kipindi cha Novemba 2025 hadi Aprili 2026, ikionya kuwa maeneo mengi ya nchi yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani, hali inayoweza kuathiri sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chan’ga, ametoa tahadhari na ushauri kwa wadau wa sekta mbalimbali kufuatilia kwa karibu taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao
Amesema inaonekana kuwa mvua hizo zitahusu mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe, Rukwa, Ruvuma, Mtwara, Lindi, pamoja na kusini mwa mkoa wa Morogoro.
Mwenendo wa Mvua za Msimu
Dkt. Chan’ga ameeleza kuwa mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya tatu na ya nne ya Oktoba 2025 katika mikoa ya Tabora, Katavi na Kigoma, na kusambaa katika maeneo mengine ya kusini na nyanda za juu kusini magharibi kufikia wiki ya pili hadi ya tatu ya Novemba 2025.
Kwa mujibu wa utabiri huo, mvua zinatarajiwa kumalizika kati ya wiki ya nne ya Aprili na wiki ya kwanza ya Mei 2026, huku kipindi cha nusu ya pili ya msimu (Februari–Aprili 2026) kikitarajiwa kuwa na mvua nyingi zaidi kuliko nusu ya kwanza.
Aidha Dkt. Chan’ga alibainisja kuwa pamoja na mvua kuwa chache, vipindi vifupi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza katika baadhi ya maeneo na kusababisha athari kama mafuriko na maporomoko ya ardhi.
Sababu za Hali Hiyo
Kwa mujibu wa maelezo ya wataalamu wa hali ya hewa, mwenendo wa mvua za mwaka huu umechangiwa na mabadiliko ya joto katika bahari kuu duniani.
TMA imesema joto la bahari katika eneo la Tropiki ya Kati ya Pasifiki linatarajiwa kuwa la wastani hadi chini ya wastani, huku Bahari ya Hindi na Atlantiki zikionesha tofauti za joto zinazoweza kudhoofisha msukumo wa hewa yenye unyevunyevu kuelekea Tanzania.
“Hali hii inatarajiwa kupunguza mvua katika maeneo mengi ya nchi, hususan kanda ya kati, magharibi, nyanda za juu kusini magharibi na ukanda wa pwani ya kusini,” imesema taarifa ya TMA.
Athari Zinazotarajiwa
TMA imesema hali ya mvua chache inaweza kusababisha upungufu wa unyevu kwenye udongo, hali itakayopunguza ukuaji wa mazao na mavuno. Pia, upungufu wa maji kwenye mito na mabwawa unaweza kuathiri upatikanaji wa maji kwa matumizi ya nyumbani, kilimo, mifugo na uzalishaji wa umeme.
Kilimo na Chakula
Mvua za chini ya wastani zinatarajiwa kuathiri mazao ya mvua moja kwa mwaka. Wakulima wamehimizwa kutumia mbegu zinazokomaa haraka, kuhifadhi maji shambani na kufuata ushauri wa maafisa ugani.
Aidha, TMA imeonya kuhusu ongezeko la wadudu waharibifu kama panya na mchwa kutokana na ukame.
Mifugo na Uvuvi
Upungufu wa maji na malisho unatarajiwa kuathiri wafugaji, na TMA imeshauri kuweka mipango ya kuhifadhi maji na chakula cha mifugo mapema.
Kwa wavuvi, imependekezwa kufuatilia kwa karibu taarifa za hali ya hewa ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa vipindi vya mvua kubwa.
Utalii na Wanyamapori
Hifadhi na mapori ya akiba yanatarajiwa kukabiliwa na upungufu wa malisho na maji kwa wanyamapori, hali inayoweza kuongeza migongano kati ya wanyamapori na jamii zinazozunguka maeneo hayo.
Nishati, Maji na Madini
Kiwango kidogo cha maji katika mabwawa kinaweza kupunguza uzalishaji wa umeme wa maji, huku shughuli za madini zinazotegemea maji zikitarajiwa kuathirika.
TMA imependekeza uvunaji wa maji ya mvua na matumizi endelevu ya vyanzo vya maji.
Ujenzi na Usafiri
Sekta hizi zinatarajiwa kunufaika na kupungua kwa mvua, lakini vipindi vya mvua kubwa vinaweza kusababisha uharibifu wa miundombinu. Wadau wametakiwa kufanya matengenezo ya kinga na ukaguzi wa mara kwa mara.
Afya na Maafa
Upungufu wa mvua unaweza kulazimisha jamii kutumia maji yasiyo safi, hivyo kuongezeka kwa magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.
TMA imeshauri serikali za mitaa na sekta ya afya kuhamasisha jamii kutibu maji na kuhakikisha upatikanaji wa dawa muhimu.
Pia, TMA imesisitiza haja ya kuimarisha Kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi zote za utawala ili kujiandaa kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza, zikiwemo mafuriko na ukame.
Wito kwa Vyombo vya Habari na Umma
TMA imeitaka jamii kufuatilia kwa ukaribu utabiri wa kila siku, wa siku kumi na wa kila mwezi kutoka Mamlaka hiyo, ili kupanga shughuli za kiuchumi kwa ufanisi.
Aidha, imekumbusha kuwa ni kosa kisheria kusambaza taarifa za hali ya hewa kutoka vyanzo visivyo rasmi, kwa mujibu wa Sheria ya TMA Na. 2 ya mwaka 2019.
Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa za marejeo za msimu ili kusaidia wadau wote kupanga mipango yao kwa ufanisi.