Mwandishi Wetu,
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mheshimiwa Jabiri Omari Makame, amewataka wakulima kote nchini kutumia mbolea kwa kuzingatia afya ya udongo ili kuongeza tija na kulinda ardhi kwa vizazi vijavyo.
Alisema matumizi ya mbolea yasiyoendana na hali halisi ya udongo yanapunguza ufanisi na kuharibu mazingira.
Akizungumza tarehe 3 Agosti 2025 katika banda la TFRA kwenye Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, Mhe. Makame alisisitiza kuwa vifaa vya kupima afya ya udongo vinapatikana katika kila halmashauri, hivyo wakulima wanapaswa kuvitumia ili kuwa na hakika na aina ya mbolea wanayoitumia.
Aidha, aliwataka wakulima kuwa na tabia ya kupima udongo mara kwa mara ili kupata taarifa sahihi zitakazowawezesha kuchagua aina sahihi ya mbolea kwa ajili ya mazao yao, na kubainisha kuwa hili ni jukumu la msingi kwa kila mkulima.
Katika hatua nyingine, Mhe. Makame alitoa onyo kali kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na utoroshaji au uchakachuaji wa mbolea, na kueleza serikali haitasita kuwachukulia hatua kali wahusika wa vitendo hivyo vinavyohujumu juhudi za serikali za kukuza sekta ya kilimo.
Alimalizia kwa kusisitiza kuwa serikali kwa kushirikiana na taasisi kama TFRA itaendelea kusimamia ubora wa pembejeo, kutoa elimu kwa wakulima na kuweka mazingira bora ya kuhakikisha mbolea bora na salama inawafikia walengwa kwa wakati ili kuongeza uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula.


