TUUNGANE NA MHE. RAIS SAMIA KATIKA KUHIFADHI MALIASILI: CP. WAKULYAMBA

 

…………………

Na Sixmund Begashe – Mugumu

Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea na jitihada za kuimarisha mahusiano mema na wananchi wanaoishi jirani au pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti ili kuongeza nguvu katika uhifadhi na kuondoa Migongano baina ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Maliasili Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba katika kikao maalum na Madiwani, Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Serengeti pamoja na Maafisa waandamizi wa Jeshi la Uhufadhi wa Taasisi za TANAPA na TAWA.

Katika kuendeleza jitihada hizo CP. Wakulyamba amebainisha kuwa Wizara inaratibu mkakati wa kuwa na Askari wa Uhifadhi katika ngazi ya Kata zinazopakana na Hifadhi ili kuimarisha mahusiano mema baina ya wananchi na Hifadhi za Taifa na pia kusaidia upatikanaji wa Taarifa kwa haraka zinazohusu changamoto zozote za kiuhifadhi na kuzipatia utatuzi wa haraka.

CP. Wakulyamba ametoa wito kwa wananchi kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndie Mhifadhi namba moja wa uhifadhi wa Maliasili nchini, kwa kutovamia maeneo yaliyohifadhiwa kisheria ili kuhakikisha migongano baina ya Wanyamapori wakali na waharibifu inamalizika.

“Nasisitiza, Uongozi wa Hifadhi lazima kuhakikisha mnafanya vikao vya mara kwa mara na wananchi au viongozi wao ili kupata Taarifa muhimu kutoka kwao na pia kutoa elimu ya uhifadhi. Hii itasaidia kuimarisha mahusiano mema na wananchi” Alisisitiza CP. Wakulyamba

Naye Diwani Kata ya Nyansurura Mhe. Josephat Ryoba Seronga ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa jitihada kubwa inayofanya katika kupambana na changamoto za Wanyamapori wakali na waharibifu kwa wananchi wa vijiji jirani na maeneo yaliyohifadhiwa katika Wilaya ya Serengeti.

Aidha, ameiomba Wizara hiyo kuharakisha mchakato wa kuweka Askari wa Uhifadhi katika Kata zinazopakana na Hifadhi ili kusogeza huduma za uhifadhi jirani zaidi na wananchi.

Kikao hicho kilichoudhuriwa pia na Katibu Tawala Wilaya ya Serengeti Bi. Angela Marco Lubella, Maafisa waandamizi kutoka TANAPA, TAWA, TFS, Kamati ya Usalama, Waheshimiwa Madiwani kutoka Kata za Kisandura, Mbalibali, Ikoma, Nyasurura na Machochwe, kililenga kuzitazama changamoto za kiuhifadhi na kuweka mikakati ya pamoja ya kuitatua kwa maslai mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post