Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi maalumu ya matibabu kwa wananchi wa mkoa wa Mbeya. Jumla ya watu 751 walipata huduma za uchunguzi na matibabu watu wazima walikuwa 720 na watoto 31.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Anna Nkinda akigawa vipeperusha vya lishe na shinikizo la juu la damu kwa wananchi wa mkoa wa Mbeya waliofika kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zilizokuwa zinatolewa katika kambi maalumu ya matibabu iliyofanyika katika viwanja vya City Park Garden. Jumla ya watu 751 walipata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi hiyo.
Afisa Muuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) akimpima uwiano baina ya urefu za uzito mkazi wa Mbeya aliyefika kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zilizokuwa zinatolewa katika kambi maalumu ya matibabu iliyofanyika katika viwanja vya City Park Garden. Huduma hiyo ilitolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Wakazi wa mkoa wa Mbeya wakisubiri kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zilizokuwa zinatolewa katika kambi maalumu ya matibabu iliyofanyika katika viwanja vya City Park Garden. Huduma hiyo ilitolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ameitaka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuendelea kutoa elimu kwa umma ya magonjwa ya moyo ili wananchi wawe na ufahamu wa magonjwa hayo
Maagizo hayo ameyatoa jana jijini Mbeya wakati akipewa taarifa ya kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya moyo, huduma iliyotolewa kwa washitiri wa mkutano wa 109 wa wadau wa Elimu kwa Umma ulioandaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na wananchi wa mkoa wa Mbeya.
Mhe. Dkt. Mpango alisema ni muhimu kwa wataalamu hao kwenda kwenye vyombo vya habari kutoa elimu itakayowasaidia wananchi kujua dalili za magonjwa ya moyo na madhara ya ugonjwa huo.
“Ninajua mnatoa elimu kwa umma kuhusu magonjwa ya moyo ila ongezeni juhudi zaidi ya kwenda katika vipindi mbalimbali vya TBC mkatoe elimu ili wananchi waone umuhimu wa kupima afya zao na kuchukuwa hatua”, alisisitiza Mhe. Dkt. Mpango.
Akitoa taarifa ya upimaji huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge, Daktari bingwa wa moyo kwa watoto Stella Mongella alisema kwa siku tano waliona watu 751 kati ya hao watu wazima walikuwa 720 na watoto 31, waliohitaji kufanyiwa uchunguzi zaidi na kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI walikuwa 50 kati ya hao watu wazima 42 na watoto nane.
Dkt. Stella alisema kati ya watu waliowaona 135 walikuwa hawajijui kabisa kuwa na magonjwa ya moyo lakini baada ya kufanyiwa upimaji walikutwa na matatizo na kuanzishiwa dawa za kutumia na watu 86 walipata elimu ya mtu mmoja mmoja ya lishe bora.
“Watu wazima wengi tuliwakuta na tatizo la shinikizo la juu la damu, kutanuka kwa misuli ya moyo na baadhi mishipa ya damu ya moyo imeziba kwa upande wa watoto tuliwakuta na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa katika mpangilio wake”.
“Changamoto kubwa tuliyoiona ni wagonjwa wengi kuacha kutumia dawa za shinikizo la juu la damu pindi wanapojisikia kupata naafuu pia wananchi wengi hawana bima za afya hivyo basi ninaamini kuanza kutumika kwa bima ya afya kwa wote kutawasaidia watu wengi kuwa za bima ya afya”, alisema Dkt. Stella.
Ili kusogeza upatikanaji wa huduma za matibabu ya kibingwa ya moyo kwa wananchi Taasisi hiyo ilianzisha huduma za tiba mkoba zijulikanazo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services kwa kuwafuata wananchi mahali walipo. Kwa mwaka jana ilitolewa katika mikoa 10 na maeneo ya kazi nane ambapo watu 12,809 watu wazima wakiwa 10,863 na watoto 1,946 walifanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo.
Kati ya hao 4,613 watu wazima wakiwa 4,405 na watoto 208 walikutwa na matatizo mbalimbali ya moyo na kuanzishiwa matibabu. Wagonjwa 1,350 watu wazima 1,192 na watoto 158 walikutwa na matatizo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa na kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI.
Kambi hiyo ya siku tano ya uchunguzi na matibabu ya moyo iliyofanyika katika viwanja vya City Park Garden jijini Mbeya ilifanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, MZRH na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).