WATUMISHI BRELA WASISITIZWA UADILIFU NA NIDHAMU KATIKA KAZI

 


Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa akifafanua jambo wakati wa kikao maalumu na Wafanyakazi wa Taasisi hiyo  kwa lengo la kukumbushana majukumu na kusikiliza changamoto na kuzitatua kilichofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

NA MWANDISHI WETU

OFISA Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Godfrey Nyaisa amewataka watumishi wa taasisi hiyo kuzingatia maadili na kuweka nidhamu katika utendaji kazi ili kuongeza ufanisi katika kutoa huduma kwa  wananchi.

Nyaisa ameyasema hayo wakati wa kikao maalumu na watumishi wote wa BRELA kilichofanyika katika ukumbi wa PSSSF jijini Dar es Salaam kwa  lengo la kukumbushana majukumu, kusikiliza changamoto za kiutendaji na kuzitatua pamoja na kuwapongeza wafanyakazi bora na kuwa aga watumishi walio staafu.

“Napenda kuwasisitiza sana suala la nidhamu ya kazi, tujenge utamaduni wa kuheshimu nafasi  tulizonazo na tuwe waadilifu mahala pa kazi ili hata ukienda taasisi nyingine nje ya BRELA waone kweli umejifunza kazi na unaiweza kufanya kwa ufanisi” alisema Nyaisa

Aliongeza kuwa. kila mmoja atambue wajibu wake na kuutekeleza, na kuwataka wafanyakazi hao watambue kwamba juhudi za mfanyakazi mmoja mmoja ndizo zinazompa nafasi Afisa Mtendaji Mkuu kuonekana kuwa anafanya kazi na kuipa sifa Taasisi kwa ujumla.


Aidha Nyaisa amesema, ataendelea kufanyia maboresho ya kiutendaji changamoto zilizopo na kuwataka wafanyakazi kuendelea kuwa wavumilivu wakati misingi ya maboresho ikiendelea kuwekwa kwa ajili ya watumishi wote.

Kikao hicho kilifuatiwa na hafla ya kuwapongeza wafanyakazi bora na hodari waliofanya vizuri kwa mwaka 2023/2024 ambao walitunukiwa vyeti na zawadi kwa wafanyakazi bora huku mfanyakazi Hodari wa Taasisi  akipata cheti na TZS. Milioni tatu.

Watumishi bora waliopata zawadi na cheti ni Vicente Nyanje, Abdulkarim Nzori, Boniface Ngugi, Abas Cothema, Gwamaka Mwankenja, Mwajabu Goma, Swedi Jabiri na Onesmo Mushi ambaye pia amekuwa mtumishi Hodari wa mwaka na kuondoka na TZS. Milioni tatu za Kitanzania.


Katika kikao hicho pia watumishi waliostaafu waliagwa na kupongezwa kwa mchango wao walioutoa kwa taasisi,  ambapo kwa kutambua hilo Ofisa Mtendaji Mkuu Bw. Godfrey Nyaisa alitoa zawadi maalumu ya vocha yenye thamani ya shilingi milioni moja kwa kila mtumishi ambayo watakwenda kufanya manunuzi ya kitu chochote.

Wafanyakazi hao waliostaafu utumishi wao kwa mujibu wa sheria ni pamoja na Deo Meela, Andrew Mkapa, Bi.Gloria Binamungu na Gloria Mbilimonywa    

Sambamba na hayo, Nyaisa. Aliwapongeza pia watumishi ambao wamekuwa wakiandika makala maalumu za kitaalam kuhusu majukumu yanayofanywa na BRELA kwa lengo la kutoa elimu kwa umma na kutoa rahi kwa watumishi wingine kufanya hivyo ili umma uweze kujua shughuli mbalimbali za kiutendaji na hivyo wafanyabiashara kuweza kurasimisha biashara zao.

Watumishi waliotambuliwa mchango wao ni  pamoja na Stanslaus Kigosi, Isdor Nkindi, Menrad Rweymamu, Abdul Songoro, Sweetness Madata, Calvin Rwambogo, Andrew Mares na Tawi Kilumile.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw.Godfrey Nyaisa akimkabidhi cheti cha kutambua mchango wake, Deo Meela ambaye amestaafu utumishi kwa mujibu wa sheria  katika hafla iliyofanyika baada ya  kikao na wafanyakazi  kwa lengo la kukumbushana majukumu na kusikiliza changamoto na kuzitatua kilichofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wafanyakazi hodari kutoka Idara na Vitengo vya taasisi  baada ya kuwapongeza katika hafla iliyofanyika baada ya  kikao na wafanyakazi  kwa lengo la kukumbushana majukumu na kusikiliza changamoto na kuzitatua kilichofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Post a Comment

Previous Post Next Post