
Kamishna msaidizi mwandamizi anayesimamia sehemu ya huduma za utalii,Mariam Kobelo akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha .

Wanawake hao wakiwa katika picha ya pamoja bada ya kikao na waandishi wa habari mkoani Arusha
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .Katika kuelekea siku ya wanawake duniani itakayofanyika machi 8 ,mkoani Arusha Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kwa kushirikiana na kampuni ya utalii ya Tanzanite Corporates imeandaa safari kwa ajili ya kuhamasisha utalii wa ndani kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kwa ajili ya kutembelea vivutio vya utalii itakayofanyika machi 7.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha ,Kamishna msaidizi mwandamizi anayesimamia sehemu ya huduma za utalii,Mariam Kobelo amesema kuwa,lengo la safari hiyo ni kuhamasisha utalii huku akiwataka wanawake kujitokeza kwa wingi katika siku hiyo.
“Kama mnavyojua maadhimisho ya siku ya wanawake duniani hufanyika kila mwaka tarehe 8 machi ambapo kwa mwaka huu kama tulivyotangaziwa na viongozi mbalimbali, Mkoa wa Arusha umepata heshima ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho haya kitaifa ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan”amesema.
“katika kunogesha maadhimisho ya siku hiyo Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) ikishirikiana na kampuni ya Tanzania Cooperate imeandaa safari ya kutwa (Day trip) kwa ajili ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo hifadhi ya Ngorongoro hususan Ngorongoro Crater ambapo tumeandaa kifurushi cha bei nafuu ili kuwezesha wanawake wengi kufanya utalii wa ndani katika hifadhi ya Ngorongoro kuelekea maadhimisho ya siku hiyo.”amesema Kobelo.
Amefafanua kuwa ,NCAA na Tanzania Coorporate wameandaa kifurushi cha shilingi 170,000 kwa kila mtu ambae angependa kutembelea Ngorongoro Kreta, kifurushi hicho kitajumuisha gharama za kiingilio, chai ya asubuhi, chakula cha mchana, usafiri, gharama za muongoza watalii pamoja na kila mshiriki kupewa kofia atakayovaa wakati wa safari ya Utalii.
Amefafanua zaidi kuwa , Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa kinara namba moja kutangaza Utalii wa vivutio tulivyokuwa navyo hapa nchini,kama ilivyokuwa katika Filamu ya Tanzania the Royal Tour na Amaizing Tanzania yeye ndio amekuwa Jasiri muongoza njia kutangaza utalii wa nchi yetu duniani.
Amesema kuwa,Kufuatia juhudi hizo wao kama wanawake wa Sekta ya Utalii wameamua kumuunga mkono kwa kuhamasisha wanawake wajitokeze kwa wingi kuungana katika safari hii ya kufanya Utalii Ngorongoro ambapo wanaamini wote watakaolipia kifurushi cha 170,000 kwenda kutalii Ngorongoro watapata uzoefu mzuri usiosahaulika katika Maisha yao (Unforgettable experience).
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya utalii ya Tanzanite Corporates, Elina Mwangomo amesema kuwa,kwa wote ambao watalipia kifurushi hiki kwenda Ngorongoro watarajie kuona vivutio mbalimbali vinavyojumuisha mazingira asilia, bonde maafuru la Ngorongoro ambalo ni moja ya maajabu saba barani afrika, wataona mtawanyiko wa Wanyama mbalimbali ikiwemo Wanyama wakubwa watano ambao ni Simba, chui, Faru, tembo na Nyati wakiwa katika mazingira ya asili na katika safari hii watapaka huduma ya usafiri uliopo katika kiwango kizuri na usalama wa kutosha wakati wote wa safari.
Aidha amewataka wanawake wote ambao wangependa kuungana katika safari hii kuwa safari itaanzia katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Arusha saa 11 alfajiri kwa ajili ya kwenda Ngorongoro na kurudi jioni yake ili kesho yake tarehe 8 machi, 2025 waungane na Mheshimiwa Rais na viongozi mbalimbali wa kitaifa katika kusherehekea siku ya wanawake duniani.
Ameongeza kuwa , ili kupata utaratibu wa malipo ya safari hiyo kwa wale ambao watahamasika kuunga mkono jitihada za utalii wa ndani nawaomba wawasiliane nasi kwa namba zifuatazo 0758171914 au Namba 0763 291179 kisha watapewa utaratibu.
Kwa upande wake Afisa utalii kutoka ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Arusha ,Tabea Mollel kwa pamoja wameungana na wadau hao katika kufanikisha safari hiyo ikiwa ni pamoja na kumuunga mkono Rais Samia katika maswala ya utalii huku akitoa wito kwa wanawake wote kuhakikisha wanaungana pamoja kufanikisha siku hiyo.