WAFANYABIASHARA WA KARIAKOO WATAKIWA KUWAFICHUA WAKWEPA KODI

     

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amewataka Wafanyabiashara wa Kariakoo Jijini Dar es Salaam kuwafichua watu wanaokwepa Kodi kwa namna mbalimbali ili wachukuliwe hatua na kuleta ushindani uliosawa sokoni.

Akizungumza leo tarehe 04/02/2025 wakati wa kuwasimika Mabalozi wa nyumba kwa nyumba kwaajili ya kusimamia zoezi la kurasimisha biashara ili kuhakikisha kila mmoja anasajiliwa na kupatiwa TIN namba na analipa Kodi kwa hiari katika soko la Kariakoo Mwenda amesema wakwepa Kodi hawatakiwi kufumbiwa macho.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema Mabalozi hao watasaidia katika kuhakikisha kunakuwepo na usawa kwenye kulipa Kodi kwa hiari kwa kuwezesha watu wote wanaofanya biashara Kariakoo kusajiliwa na kulipa Kodi inayostahili hali ambayo itaweka ushindani uliosawa sokoni.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema jukumu kubwa la TRA ni kusimamia ustawi wa biashara ili ziendelee kukua na kuhakikisha kuwa hakuna biashara inayokufa na kwa Kariakoo ni eneo muhimu la biashara linalogusa mikoa yote na nchi jirani.

Amesema Kariakoo ni wachangiaji wakubwa wa Kodi kutokana na kuwepo kwa Walipakodi wadogo, wa kati na wakubwa hivyo ipo haja ya TRA kuwa karibu nao na kuwasaidia kuondoa changamoto zinazowakabili.

Bw. Mwenda amesema changamoto za kisera zinazowakabili walipakodi tayari zimeundiwa Tume na Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na zinafanyiwa kazi huku zile zinazotakiwa kushughulikiwa na TRA ambazo ni za kimfumo nazo zikiwa zinatatuliwa na Mamlaka yenyewe.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema milango yake ipo wazi muda wowote kwaajili ya Walipakodi na yupo tayari kuwasikiliza kwa lengo la kuboresha mazingira yao biashara.

“Rais Dk . Samia Suluhu Hassan aliponiapisha alinipa majukumu na hayo ndiyo nayasimamia ikiwemo kusimamia na kukuza uendelezaji wa biashara na ustawi wake pamoja na kukusanya Kodi kwa hiari pasipo kutumia nguvu, na jambo la heri mmekuwa tayari wakati wote kulipa Kodi na hata Wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Wamachinga nao leo wamenithibitishia kuwa wapo tayari kulipa Kodi ” CG Mwenda.

Amewataka kuwafichua wote wanaokwepa Kodi pamoja na wageni wanaofanya biashara zinazotakiwa kufanywa na wazawa maana vitendo hivyo vimekuwa vikidhoofisha ushindani ndani ya soko.

Kuhusu Wamachinga kwenda Jangwani kama walivyoahidiwa na Mhe. Rais Dk. Samia, Bw. Mwenda amesema watahakikisha wanaweka mazingira rafiki.

Bw. Mwenda amesema hakuna changamoto yoyote ya walipakodi nchini itakayokosa majibu huku akigusia suala la mizigo ya Wafanyabiashara wa Kariakoo iliyokwama Bandarini ambayo iliagizwa na Mapema Cargo na kumuagiza Naibu Kamishna wa Forodha kushughulikia changamoto hiyo kwa haraka na kuwapatia Wafanyabiashara hao mizigo yao waendelee na biashara.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Ilala Bw. Edward Mpogolo amesema wanaandaa kanzi data ya Wafanyabiashara wote wa Kariakoo na kuweka utaratibu wa pamoja na TRA katika kuwasajili Wafanyabiashara ili kuwapunguzia safari ya kuwafuata ofisini wakati wakijiandaa kuanza kufanya biashara saa 24.

Mpogolo amesema kwa Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda kwenda Kariakoo kirafiki ni jambo ambalo linaonyesha uhusiano na ushirikiano wa karibu baina ya TRA na Wafanyabiashara na linaashiria kuwepo kwa ongezeko la mapato yanayotokana na Kodi.

Severin Mushi ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo ambaye amesema kuwa wameamua kuweka Mabalozi katika kila nyumba ili wasaidie kusajili Wafanyabiashara na kuwezesha kila mwenye biashara Kariakoo kuwa na TIN namba na kulipa Kodi ili kuweka usawa katika ulipaji wa Kodi.

Severin amesema kila panapotokea changamoto wamekuwa wakishirikiana na TRA kuzitatua na kuweka mazingira bora kwa Wafanyabiashara ndani ya soko hilo.

Naye Kiongozi wa Wamachinga Steven Lusinde amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kulijali kundi lao huku akimuahidi Kamishna Mkuu Mwenda kuwa wapo tayari kulipa Kodi.

Post a Comment

Previous Post Next Post