Mhe. Samwel M. Maneno, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali akiangalia moja ya mashuka yanayotengenezwa katika moja ya kiwanda cha mashuka ambacho watumishi wa ofisi ya Mwanasheria mkuu wa Seeikali walitembelea kuona namna kinavyofanya kazi.
Bw. Onorius Njole, Mwandishi Mkuu wa Sheria akizungumza katika kikao mara baada ya watumishi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwasili katika Kongani ya Viwanda mkoani Pwani.
Bw. Buji Banpebuye Mkurugenzi wa Divisheni ya Mipango, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali akichangia maoni katika kikao hicho.
……………….
Na Mwandishi Wetu
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imewasihi viongozi wa serikali wanaohusika katika uandaaji wa miradi na mikataba kuhakikisha wanazingatia maoni na ushauri unaotolewa na ofisi hiyo ili kuimarisha utekelezaji wa miradi kwa ufanisi na kuzingatia sheria za nchi.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samwel Maneno, akizungumza na Full Shangwe Blog leo baada ya ziara katika Kongani ya Viwanda inayojengwa Kibaha, Mkoani Pwani, amesema jukumu kuu la ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni kuhakikisha serikali inazingatia misingi ya kisheria katika masuala yote yanayohusu mikataba na miradi.
“Tunazingatia misingi ya kisheria kuhakikisha kwamba mikataba iliyotayarishwa inafuata sheria za nchi na kimataifa. Pia tunaangalia maeneo yenye vihatarishi au vifungu ambavyo havifai kuwepo kwenye mikataba ili kuepuka changamoto za utekelezaji,” alisema Mhe. Maneno.
Mhe. Maneno alisisitiza kuwa kwa mujibu wa sheria, maoni na ushauri wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni lazima yazingatiwe na viongozi wa serikali. Alisema kufuata ushauri wa kisheria kunahakikisha kuwa mikataba inatekelezwa kwa usahihi na kwamba viongozi wanabaki salama kisheria.
“Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni mshauri mkuu wa masuala ya kisheria kwa serikali. Tunatoa wito kwa viongozi kuitumia ofisi yetu kila wanapohitaji msaada wa kisheria katika maeneo yao ya kazi,” aliongeza.
Mhe. Maneno alifafanua kuwa kusaini mikataba ni hatua ya awali tu, lakini kuhakikisha utekelezaji wake kwa ufanisi kunahitaji umakini mkubwa. Alieleza kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inahakikisha kila anayehusika katika utekelezaji wa mikataba anatimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.
“Taratibu za kisheria zinapaswa kufuatwa ili kushughulikia changamoto yoyote inayojitokeza katika utekelezaji wa miradi,” alisema.
Kuhusu thamani ya fedha katika miradi, Mhe. Maneno alisema kuwa ofisi yake imeanzisha utaratibu wa kutembelea miradi mikubwa ya kitaifa na kimataifa ili kuhakikisha utekelezaji unafuata mikataba.
“Tumetembelea miradi kama Bwawa la Mwalimu Nyerere, Reli ya SGR, na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato. Leo tumetembelea Kongani ya Viwanda Kibaha, ambapo tumeshuhudia utekelezaji wa mikataba ya uwekezaji,” alisema.
Mhe. Maneno ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa ufanisi mkubwa. Alisema miradi hiyo inatekelezwa kupitia mikataba zaidi ya 5,000 kila mwaka wa bajeti, ikiwemo miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja, shule, hospitali, na maji.
“Usimamizi wa miradi hii mingi unahitaji mfumo wa kupokea taarifa kwa wakati na kutoa ushauri wa kisheria kwa haraka. Tuna mawakili walioko katika ofisi za serikali kote nchini kuhakikisha huduma za kisheria zinapatikana kwa wakati,” alihitimisha.