DAWASA YAWEKA WAZI MIKAKATI YA KUIMARISHA HUDUMA YA MAJI


 Mwandishi Wetu,

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imesema inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ya kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo ya jirani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya uhakika na endelevu.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya miradi hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, amesema Mamlaka imewekeza katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya maji ili kuondoa changamoto za muda mrefu na kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

“Miongoni mwa miradi muhimu iliyotekelezwa ni Mradi wa Bangulo, ambao umeboresha kwa kiwango kikubwa huduma ya maji kwa wakazi wa Bangulo, Kinyerezi, Ulongoni A na Ulongoni B pamoja na maeneo ya Ukonga, Segerea, Ubungo, Kisarawe na Temeke,” amesema Mhandisi Bwire.

Ameeleza kuwa mradi huo wa gharama ya bilioni 36.9 umechangia kuongeza upatikanaji wa maji na kupunguza changamoto zilizokuwa zikiwakabili wananchi kwa muda mrefu.

Aidha, amesema DAWASA imekamilisha pia utekelezaji wa mradi wa kituo cha kusukuma maji (booster pump) cha Golani, kinachohudumia maeneo ya Golani, Saranga, Ukombozi na maeneo ya jirani.

Kwa mujibu wa Mhandisi Bwire, kituo hicho chenye uwezo wa kusukuma lita 150,000 za maji kwa saa kimejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 291 na kinanufaisha zaidi ya wakazi 5,000.

“Ujenzi wa kituo hiki ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha hata maeneo yenye miinuko yanapata huduma ya maji ya uhakika wakati wote,” amesema.

Katika hatua nyingine, DAWASA imeendelea kuboresha huduma ya maji kupitia Mradi wa Mshikamano, unaowanufaisha wakazi wa Mbezi, Makabe, Msakuzi Kaskazini na Msakuzi Kusini kwa kuimarisha usambazaji wa maji katika maeneo hayo.

Mhandisi Bwire amesisitiza kuwa Mamlaka itaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ya maji ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi, salama na ya kutosha kwa matumizi ya kila siku.

Post a Comment

Previous Post Next Post