Mwandishi Wetu,
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent, ameipongeza timu ya Mamlaka hiyo kwa mafanikio makubwa ya kutetea kombe la mchezo wa pool table kwa mara ya tatu mfululizo katika mashindano yaliyoandaliwa na Shirikisho la Michezo ya Mashirika ya Umma, Taasisi, na Makampuni Binafsi (SHIMMUTA).
Joel ametoa pongezi hizo leo tarehe 12 Desemba, 2024 alipopokea Rasmi kombe la mchezo huo lililokabidhiwa kwa Mamlaka siku ya kilele cha mashindano hayo Mjini Tanga.
Joel amesema, ushindani wa msimu huu ulikuwa mkali zaidi kutokana na kuongezeka kwa taasisi nyingine 31, lakini juhudi za wachezaji wa TFRA zilipelekea mafanikio hayo makubwa.
Aidha, ameweka wazi kuwa msimu ujao Mamlaka hiyo itaweka mikakati thabiti zaidi ili siyo tu kutetea vikombe vilivyopo bali pia kurejesha vikombe vingine vilivyopotea, huku wakipanua wigo wa kushiriki michezo mingine kama mpira wa miguu na mpira wa kikapu kwa wanawake.
Kwa upande wake, Afisa Utumishi na Mwenyekiti wa Michezo wa TFRA, Frank Kapama, ameishukuru taasisi kwa ushirikiano uliotolewa katika kipindi chote cha mashindano hayo.
Frank alisisitiza kuwa timu yao ina ari kubwa ya kuendelea kupambana na kuongeza vikombe msimu ujao, akisema: "Hii ni mwanzo tu, tutahakikisha TFRA inaendelea kung'ara na kuitangaza vyema taasisi yetu kupitia michezo."
Kwa mara nyingine, TFRA imeonyesha kuwa mbali na majukumu yao makuu ya kudhibiti tasnia ya mbolea, wanazingatia pia umuhimu wa michezo kama sehemu ya kuimarisha mshikamano na kuitangaza taasisi.