Wajitokeza kwa wingi kujipatia majiko ya gesi ya ruzuku
Wakazi wa Wilaya ya Ngorongoro Mkoani Arusha wameitikia wito wa kutumia Nishati Safi ya Kupikia ikiwa ni hatua ya kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kulinda afya na kutunza mazingira.
Hayo yamedhihirika Desemba 8,2024 Wilayani Ngorongoro wakati wa utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa majiko ya gesi yanayotolewa kwa bei ya ruzuku ya 50% na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa ushirikiano na Kampuni ya Lake Gas wilayani humo.
Akizungumza wakati wa zoezi la usambazaji na uuzwaji wa majiko hayo ya ruzuku wilayani humo, Msimamizi wa Mradi wa REA Kanda ya Kaskazini (Kilimanjaro na Arusha), Mhandisi Gift Kombe aliwasisitiza wananchi kuzingatia elimu inayotolewa ya matumizi sahihi ya majiko hayo ili yaweze kuleta tija inayokusudiwa ikiwa na kuendelea kujaza mitungi hiyo pindi inapoisha.
Wananchi wilayani humo kwa nyakati tofauti walishukuru kwa kufikiwa na mradi na waliahidi kuwa mabalozi kwa wananchi wengine ambao hawakupata fursa ya kufika kupata huduma.
"Kwakweli hili ni jambo jema ila bahati mbaya si wananchi wote wameweza kufika hapa; tutaendelea kuhamasishana katika matumizi ya nishati safi ya kupikia," alisema Samwel Maganila mkazi wa Wasso Mashariki, Ngorongoro.
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 ambao ulizinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mwezi Mei mwaka huu.