Na WAF - DODOMA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amesema matumizi sahihi ya kemikali ni kiungo muhimu ili kuchagiza maendeleo nchini na Duniani kwa ujumla kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Dkt. Jingu ametoa kauli hiyo Desemba 11, 2024, mkoani Dodoma wakati akifungua kikao cha wadau wa kemikali nchini kilichoandaliwa na ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kuwashirikisha zaidi ya wataalam 187 kutoka makampuni na Tasisi mbalimbali ya nchini.
“Maendeleo makubwa tunayoyapata kwenys sekta zote mchango wa sekta ya kemikali ni mkubwa, kwahiyo matumizi sahihi ya kemikali ni kiungo muhimu,” amesema Dkt. Jingu.
Dkt. Jingu amewataka wakemia binafsi na wa Serikali kuhakikisha wanazingatia miongozo, kanuni na sheria kwa kuongeza umakini wa matumizi sahihi ya kemikali ili kuepusha madhara kwa binadamu na mazingira.
“Nitoe rai kwa sisi wote kuhakikisha tunatumia kemikali vizuri kwa matumizi sahihi ya kwa ajili maendeleo ya makampuni yetu, nchi yetu, watu wetu na jamii zetu kwa ujumla na kuepusha madhara kwa watu na mazingira kwa ujumla,” amesema Dkt. Jingu.
Dkt. Jingu pia ameitaka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuendelea kutoa elimu na mafunzo kwa watendaji na wasafirishaji wa kemikali kuhusu matumizi sahihi ya kemikali kulingana na shughuli wanazozifanya bila kusahau matumizi ya vifaa kinga ili kujiepusha na vilema vya kudumu na athari zinazoepukika.
“Ofisi ya Mkemia iendelee zaidi kwa kufanya tathmini za mara kwa mara ya vifaa vya usalama katika maeneo yetu, itasaidia kuyaona maeneo ya shida na yenye ukakasi na kuendelea kuzingatiwa kanuni na miongozo,” amesema Dkt. Jingu.
Kwa upande wake Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko awali akimkaribisha Katibu Mkuu amesema lengo la mafunzo hayo kwa wadau ni kuhakikisha kuwa matumizi ya kemikali yanakuwa salama wakati wote ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza katika afya za binadamu na mazingira.