Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Mwenda amesema Mamlaka hiyo haitasita kuwachukulia hatua za kisheria wafanyabiashara wote wanaokiuka matumizi sahihi ya Mashine za Kielekitroniki EFDs.
Akizungumza katika Kikao cha pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kamishna Mkuu wa TRA Mwenda amesema timu ya Wataalam wa Mamlaka ya Mapato wapo mtaani kufanya ukaguzi wa matumizi ya Mashine za EFD na hii inatokana na kuwepo kwa baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu wanaotoa risiti feki.
"Ukikutwa unatoa risiti zisizokuwa halisi (feki) huo ni wizi kama ulivyo wizi mwingine na utachukuliwa hatua za kisheria hivyo wahimize anaojihusisha na vitendo hivyo waache kabla hatujawafikia" Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Mwenda.
Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Mwenda amesema imezuka tabia kwa baadhi ya wafanyabiashara kuuza risiti za EFD kinyume cha sheria maana risiti hizo haziuzwi bali zinatolewa baada ya kununua bidhaa.
Aidha Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Mwenda amewashukuru Walipakodi wa Tanzania wanaolipa kodi kwa uaminifu na kuahidi kuendelea kutolewa kwa elimu ya Mlipakodi nchini.