Wanamichezo TFRA watakiwa kuiwakilisha vema Taasisi SHIMMUTA

Mwandishi Wetu,

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania, (TFRA), Dkt. Asheri Kalala amewataka watumishi wanaokwenda kushiriki michezo inayoandaliwa na Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi Tanzania (SHIMMUTA) kuiwakilisha vema kwenye michezo hiyo.

Amewataka kutumia fursa hiyo kuelimisha umma juu ya matumizi sahihi ya mbolea  ili watumishi pamoja na wananchi wa mkoa huo watumie mbolea za ruzuku katika kilimo chao ili kuongeza tija.

Amesema hayo leo tarehe 8 Novemba, 2024 zilipo ofisi Za Mamlaka Temeke Jijini Dar es Salaam alipokuwa akiagana na wanamichezo walio tayari kuelekea mkoani Tanga   kushiriki mashindano ya michezo mbalimbali iliyoandaliwa na shirikisho hilo.

"Michezo ni afya, michezo itawaepusha na magojwa yasiyo ya kuambukiza hivyo mmechagua  vyema kushiriki mashindano hayo" Dkt. Kalala aliongeza

Kwa upande wake Afisa Utumishi na Mwenyekiti wa Michezo wa TFRA, Frank Kapama ameihakikishia Mamlaka kuwa maelekezo yaliyotolewa yatazingatiwa na Mamlaka itawakilishwa vyema katika michezo hii ambayo Mamlaka inashiriki kwa awamu ya tatu sasa.

Aidha, ameishukuru Menejimenti ya TFRA kwa kujali afya za watumishi kwa kuwawezesha kuwa na mwalimu wa mazoezi na zaidi kuwaruhusu kushiriki michezo ya SHIMMUTA kwa awamu nyingine.

Ameeleza kuwa,  ni matarajio ya wanamichezo kufanya vizuri zaidi ya Mwaka jana na kuipelekea Taasisi vikombe vingi zaidi. 

Amesema, Michezo ya SHIMMUTA itaanza rasmi Novemba 10 hadi Novemba 24, 2024 Mkoani Tanga, ambapo wanamichezo 22 kutoka TFRA watashiriki katika michezo ya  mpira wa kikapu, Bao, pull table Karata, Riadha, Vishale, draft pamoja na mbio za Majunia.



Post a Comment

Previous Post Next Post