REA KUSHIRIKIANA NA MKOA WA KIGOMA USAMBAZAJI WA MAJIKO YA GESI 19,530

 Kila wilaya kusambaziwa mitungi ya gesi 3,255


Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kamishna Jenerali, Mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mhe. Thobias Andengenye umesema mkoa wa Kigoma umepokea kwa mikono miwili Mradi huo wa kusambaza majiko ya gesi 19,530 ambayo yatauzwa kwa bei ya ruzuku (Nusu bei) ambapo Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imemtambulisha kampuni ya ORYX Gas Tanzania Ltd kuanza kazi hiyo mara moja.

Akiongea na Wanahabari ofisini kwake, tarehe 29 Novemba 2024, Mhe. Andengenye amesema, mkoa wa Kigoma umekuwa mstari wa mbele katika utunzaji wa mazingira kwa kuwa na misitu ya kutosha na kwamba matumizi ya majiko ya gesi yatachangia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa na kuongeza kuwa Mradi huo, utakuwa kichocheo kwa Wananchi kuendelea kutunza mazingira kwa kutokata misitu.

“Inawezekana kabisa idadi hii ya majiko ya gesi, ambayo mkoa tumepata kupitia Mrdi huu wa REA inaweza ikawa siyo toshelevu lakini, itatusaidia kupata mabalozi wa nishati safi ya kupikia kwa namna ilivyo rafiki kwa mazingira, rahisi kuitumia na kuinunua”.

“Nawapongeza REA kwa kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, nishati hii ni salama na rafiki katika utunzaji wa mazingira yetu pamoja na afya za watumiaji wa nishati safi, ” Amesema, Mhe. Thobias Andengenya.

Kwa upande wake, Mhandisi Mwandamizi Msimamizi wa Miradi kutoka REA, Deusdedith Malulu amesema fursa ya kupata jiko la gesilenye kilo sita (6) ni kwa kila Mwananchi wa mkoa wa Kigoma kinachotakiwa ni kuwa na kitambulisho cha Taifa au namba ya NIDA pamoja shilingi elfu ishirini (20,000/) amezitaja wilaya zinazonufaika na Mradi huo ni pamoja na wilaya ya Kigoma, Kibondo, Kakonko, Kasulu, Uvinza na Buhigwe.

“Kila wilaya itasambaziwa mitungi ya gesi 3,255 ya kupikia pamoja na kichomeo (Burner) kwa Wananchi kupitia kampuni ya ORYX Gas Tanzania Ltd. Tunaendelea kuhamasisha kuhusu matumizi ya nishati safi ili wajitokeze kwa wingi kununua mitungi hii, inayotolewa kwa bei ya punguzo ya asilimia 50,” ameeleza, Mhandisi, Malulu.

Ameongeza kuwa, elimu ya matumizi sahihi ya nishati safi inaendelea kutolewa kwa Watanzania ili kuhamasisha na kuchochea jamii kutumia nishati safi na salama.


Post a Comment

Previous Post Next Post