No title

 JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA 

 WIZARA YA AFYA TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MTANZANIA ALIYEUGUA UGONJWA WA MPOX AKIWA NCHINI ZAMBIA  Dodoma, Tarehe 11 Oktoba, 2024.  Ndugu wananchi, mnamo tarehe 10 Oktoba, 2024, Wizara ya Afya ilipokea taarifa iliyotolewa na nchi ya Zambia pamoja na Shirika la Habari la Reuters kuhusu Mtanzania aliyebainika kuwa na ugonjwa wa Mpox akiwa nchini Zambia.  Ndugu wananchi, Serikali imefuatilia taarifa hizo na kubaini kuwa; Mtanzania huyu mwenye umri wa miaka 32, alivuka mpaka kutoka Tanzania kwenda Zambia mnamo tarehe 02 Septemba, 2024 kupitia mpaka wa Tunduma (Tanzania) na Nakonde (Zambia) akiwa hana dalili zozote za ugonjwa wa Mpox. Mnamo tarehe 02 Oktoba, 2024, akiwa nchini humo, alikwenda katika kliniki mojawapo ambapo alipata matibabu ya awali na kuchukuliwa vipimo tarehe 04 Oktoba 2024. Tarehe 08 Oktoba, 2024 vipimo vya maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii ya Zambia vilithibitisha kuwa ni ugonjwa wa Mpox. Mgonjwa huyu bado anapata matibabu nchini Zambia. Ndugu Wananchi, dalili za ugonjwa wa Mpox huweza kuonekana kati ya siku 3 hadi 21 tangu kuambukizwa. Hivyo, kwa kuwa Mtanzania huyu alianza kuonesha dalili mwezi mmoja baada ya kutoka nchini, ni dhahiri kuwa alitoka nchini akiwa hana maambukizi.   Ndugu Wananchi, tunaipongeza nchi ya Zambia kwa kubaini ugonjwa huu mapema na kuishukuru kwa kumhudumia mgonjwa hadi sasa na pia kutoa taarifa kwa wakati. Serikali inaendelea kushirikiana na nchi ya Zambia kufuatilia hali ya mgonjwa na kuhakikisha anapona na kurejea akiwa na afya njema.   Ndugu wananchi, Wizara inapenda kuwahakikishia kuwa, bado Tanzania iko salama na hakuna mgonjwa wa Mpox aliyebainika hapa nchini hadi sasa. Wizara inaendelea kufuatilia kwa karibu kuhusu mwenendo wa ugonjwa huu na itaendelea kutoa taarifa kwa umma. Hivyo, Wizara inatoa wito kwa jamii nchini kuendelea kuzingatia kanuni za usafi, kutopeana mikono na kutoa taarifa kwa kutumia namba 199 ili kwa pamoja tuhakikishe ugonjwa huu hauingii nchini.   


Imetolewa na:

 Roida N. Andusamile

  Mkuu wa Kitengo cha  Mawasiliano ya Serikali Wizara ya Afya   

Post a Comment

Previous Post Next Post