Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amewataka Watumishi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kushirikiana ili kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Aweso ametoa kauli hiyo Leo Oktoba 23,2024 Jijini Dodoma wakati akizungumza na Menejimenti ya DUWASA katika Hafla fupi ya kukabidhi fedha taslimu shilingi milioni tano kwa Kwaya ya DUWASA ikiwa ni kutimiza ahadi yake aliyoitoa Septemba 5, 2024 wakati wa Kikao kazi cha Mamlaka na wadau.
Mhe. Aweao amewaasa watumishi kuepuka fitina, majungu, chokochoko na uzushi kwani haviwezi kujenga na badala yake wafanye kazi kwa bidii kwa taaluma zao kutafuta Suluhu ya changamoto zinazowakabili wananchi kwa kushirikiana ili huduma ya maji iwe endelevu.
Pia Waziri Aweso amewataka watumishi kutumia lugha nzuri kwa wateja wakati wa kutoa huduma na kuwapatia suluhisho ya changamoto zao.
Katika hatua nyingine Waziri Aweso ameipongeza Kwaya ya DUWASA na kuwataka kuendelea kutunga na kuimba nyimbo zinazotambulisha miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara, miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wafahamu kazi kubwa inayofanywa na serikali.
"Kwaya hii itusaidie kutangaza miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Maji, hata mimi mnanipunguzia kuongea kwani mambo mengi mnakuwa tayari mmeshayataja katika nyimbo zenu," ameeleza Aweso
Hafla hiyo imeudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Wizara ya Maji, akiwemo Naibu Waziri wa Maji, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu pamoja na Menejimenti ya Wizara ya Maji na ya DUWASA ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Aron Joseph.a