“WADAU WA MAENDELEO TUSHIRIKIANE UTEKELEZAJI WA MPANGO WA BIMA YA AFYA KWA WOTE” – MAJALIWA

Na WAF, Arusha.

Rai imetolewa kwa wadau wa maendeleo ya Sekta ya Afya kushirikiana pamoja na Serikali katika kufanikisha utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa wote pamoja na ugharamiaji wa huduma za afya ili huduma bora za afya zipatikane kwa watu wote.

Hayo yamebainishwa Oktoba 30, 2024 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa  akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Kongamano la Bima ya Afya kwa wote na Jukwaa la ugharamiaji wa huduma za afya lililofanyika Jijini Arusha.

“Ni dhahiri kuwa zinahitajika jitahada za pamoja katika utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa wote. Nitoe rai kwa wadau wote yaani jamii, wadau wa maendeleo, watoa huduma za afya, mashirika ya kijamii na mashirika ya kiraia kuendelea  kushirikiana na Serikali katika hatua zote za utekelezaji,” amesema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amesema kuwa kutokana na mabadiliko ya teknolojia ya tiba na huduma za matibabu gharama za matibabu zimeendelea kuongezeka na hivyo kuwafanya wananchi wengi kushidwa kuzimudu huku pia sekta ya afya imeendelea kukabiliwa na upungufu katika mfumo wa ugharamiaji huduma za afya.

“Hatuna budi kushughulikia changamoto hizo na kuhakikisha lengo la huduma bora za afya kwa wote linafikiwa ifikapo 2030. Ili kukabiliana na changamoto hizo, jitihada za pamoja zinahitajika kutoka kwa wadau wote, ndani ya Serikali na wadau wote wa maendeleo. Kongamano hili ni ishara ya ushirikishwaji wa wadau wote muhimu katika kuhakikisha kuwa hakuna anayeachwa nyuma katika azma ya kuwa na Taifa lenye afya bora,” amesema Mhe.  Majaliwa.

Mhe.  Majaliwa amesema kuwa Serikali imeshaanza kuchukua hatua muhimu za kujidhatiti ili kuimarisha mfumo wa ugharamiaji wa huduma za afya ikiwemo kutungwa kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ya Mwaka 2023.

Amebainisha hatua kadhaa katika kuelekea kwenye utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote kuwa ni kuendelea kuongeza kiwango cha bajeti ya Sekta ya Afya, kuanzisha mfuko kwa ajili ya kugharamia wananchi wasio na uwezo na kubainisha vyanzo mahsusi vya fedha kwa ajili ya kugharimia bima ya afya kwa wananchi wasio na uwezo ambapo katika bajeti ya mwaka 2024/2025 zimetengwa shilingi bilioni 173.5 kwa madhumuni hayo.

Mhe.Waziri Mkuu  amewataka washiriki wa Kongamano hilo kujadili na kubuni mbinu za kuimarisha ugharimiaji wa huduma za afya nchini kama vile ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi, kubuni vyanzo vipya vya fedha kwa ajili ya kugharamia huduma za afya na kuimarisha usimamizi wa fedha zinazopatika  ili zilete tija zaidi.

Aidha Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa amewataka Watanzania wote kujiandaa ili

Kujiunga na mpango wa Bima ya Afya, Serikali itakapotangaza rasmi kuanza

kuandikisha wanachama ili kila mmoja aweze kunufaika na maboresho yaliyofanywana Serikali.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa Wizara kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya imeendelea kuchukua hatua kuelekea kwenye utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote.

Hatua hizo amezitaja kuwa ni pamoja na; Kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga na bima ya afya; Kuimarisha ubora wa huduma katika vituo vya kutolea huduma ya afya nchini ; Kuendeea kusimamia ubora na weledi wa watoa huduma za afya hapa nchini ; Kuendelea kutafuta fursa mbalimbali za kuwezesha utekelezaji wa sheria hii ilkiwa ni pamoja na rasilimali fedha na rasilimali watu.



Post a Comment

Previous Post Next Post