Kamati za pembejeo za Wilaya zatakiwa kuhamasisha usajili wa wakulima ili kunufaika na mbolea za ruzuku

Na Mwandishi Wetu,

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amezitaka kamati za pembejeo za wilaya kwa kushirikiana na wenyeviti wa wilaya kuhakikisha wakulima wanajisajili kwenye daftari la mkulima na wale waliojiandikisha msimu uliopita wanahuisha taarifa zao ili wasipitwe na fursa ya mbolea za ruzuku.

Sendiga ametoa wito huo tarehe 10 Oktoba, 2024 alipokuwa akifungua maonesho ya siku nne yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania ( TFRA) kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani yanayoadhimishwa kila mwaka tarehe 13 Oktoba, duniani kote.

Sendiga amesema, awali wakulima walikuwa wakihofia kuwa watakapojiandikisha watatozwa kodi, watanyang’anywa mashamba yao lakini baada ya elimu kutolewa na na viongozi wa mikoa wakiongozwa na wakuu wa mikoa sasa wananchi wameelewa wengi wamesajiliwa na wananufaika na mbolea za ruzuku.

Akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti wa bodi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo amesema,  licha ya Mamlaka kudhibiti biashara ya mbolea nchini,  pia imekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima.

Mkurugenzi mtendaji wa TFRA, Joel Laurent amesema, kupitia maonesho hayo wakulima na wananchi watapata fursa ya kupata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea pamoja na maeneo mengine yatakayowasaidia kuongeza uzalishaji.

Amesema, mbolea ni moja kati ya pembejeo muhimu zinazohitajika katika uzalishaji wa mazao, wakati mbegu bora zikichangia takribani asilimia hamsini ya uzalishaji wa mazao mbolea huchangia kati ya asilimia ishirini hadi arobaini na asilimia zinazobaki hutokana na uzingatiaji wa kanuni bora za kilimo kwa jumla.


Post a Comment

Previous Post Next Post