Mahafali ya 20 chuo Cha Furahika kufanyika Septemba 28


Na Mwandishi Wetu,

KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Dar es Salaam, Ally Bananga anatarajia kuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 20 ya Chuo Cha Ufundi Stadi, Furahika yatakayofanyika Septemba 28, mwaka huu jijini  humo.

Taarifa hiyo, imetolewa jana jijini Dar es Salaa na Kaimu Mkuu wa chuo hicho Dkt David Msuya alipozungumza na waandishi wa habari na kufafanua kwamba katika kipindi hiki ambapo mahafali yanafanyika ndipo dirisha la usahili wa wanafunzi wapya linafunguliwa na kuwaomba wazazi kupeleka vijana wao kwa ajili ya muhula mpya wa masomo.

“Dirisha la usahili tayari limefunguliwa hivyo naomba wanafunzi waje kujisajili kwa msimu mpya na mwisho udahili ni Oktoba 30 mwaka huu kwa kozi mbalimbali hivyo ni vema wakatumia fursa hiyo mapema kabla ya dirisha halijafungwa”, amesema.

 

Dkt  Msuya ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaunga mkono lakini pia chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuendelea kuhakikisha watoto waliopo kwenye maeneo yao wanawapeleka chuoni hapo kupata elimu.

Amesema wanawapokea vijana kuanzia darasa la saba imekuwa ni faraja kwao kutokana vijana wanaotoka hapo imekuwa rahisi kupata ajira na zaidi ya asilimia 75 ya wahitimu wameajiriwa katika maeneo mbalimbali hususan ya hoteli.

Aidha ameongeza kwamba ili kuendeleza dhamira yao ya kutoa elmu bure kwa wanafunzi kwa wanafunzi wanaokidhi vigezo vya kupata elimu bure, wametia rai kwa wadau wa maendeleo hususan wa elimu kujitokeza katika kutoa misaada ya vifaa vya kufundishia ikiwemo magari hata kama mabovu watayatengeneza.

Pia amekumbusha kwa wazazi kwamba mwanafunzi wanaojiunga katika chuo hicho ambae yumo katika mpango wa elimu bure wanacholipia ni Shilingi 50, 000 kwa ajili ya usajili wa mitihani yao na si vinginevyo, hivyo anawakaribisha kutoka mikoa mbalimbali nchini na Zanzibar kujitokeza kujiunga na chuo hicho ili kupota elimu itakayowakomboa katika maisha yao.

Pia aliweka wazi kwamba kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii Zanzibar, Septemba 15 mwaka huu wataendesha semina ya kupinga katika kisiwa hicho yenye lengo la kuondoa unyanyasaji wa kijinsia miongoni mwa jamii na kuwahamasisha kujiunga na vyuo vya ufundi ili kutengeneza fikra mpya kwa ajili kuwaondoa katika mawazo yasiyo rafiki.

“Tunaamini ukatili unaanzia katika jamii, hususan kwa vijana ambao wanakuwa hawana shughuli za kufanya ambao baadhi yao wanaweza kujiiingiza katika makundo hatarishi yakiwemo ya matumizi ya dawa za kulevya, udangaji na kusababisha mimba za utotoni hivyo tukiwapa elimu ya kupinga ukatili na kuwashawishi kujiunga na vyuo vya ufundi naamini changamoto hiyo itaondoka,” amesema.

Dkt Msuya amefafanua kuwa mchakato wa kutoa elimu hiyo kupinga unyanyasaji wanaanzia katika ngazi ya Shina ambako wanaamini ndiko kuna kiini kinapoanzia na kuendelea ngazi ya Kata hadi Taifa.

Ameongeza kuwa mchakato wa kutoa elimu ya kupinga ukatili waliianza Tanzania Bara katika Kata ya Mindu, mkoani Morogoro na Chalinze mkoani Pwani na sasa wamegeukia Zanzibar na baada ya hapo watakwenda Dodoma.

Post a Comment

Previous Post Next Post