WANANCHI WA MKOA WA KATAVI WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA KATIKA MATUMIZI YA MBOLEA ZA RUZUKU

 Na Mwandishi Wetu,

Wakulima nchini wametakiwa kuzingatia kanuni bora za kilimo ikiwa ni pamoja na kuzingatia matumizi sahihi ya mbolea kwenye shughuli zao za kilimo.

Aidha, wakulima wametakiwa kuacha kilimo cha mazoea na kufuata kanuni bora za kilimo ikiwa ni pamoja na kutumia mbolea kwa usahihi.

Wito huo umetolewa na  Katibu tawala wa Mkoa wa Katavi,  Albert Msovera aliyezungumza  kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Mwanamvua Mrindoko aliyekuwa kwenye majukumu mengine wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Kilimo ni Mbolea mkoani humo tarehe 28 Agosti, 2024.

"Niwasihi wakulima wote nchini wakiwemo wa mkoa huu wa Katavi kuchangamkia fursa zinazotolewa kupitia sekta ya kilimo ili muweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali ya Jemedari Dkt. Samia Suluhu Hassan" Msovela ameongeza.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Eliurd Mwaiteleke amesema, matumizi ya mbolea kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ni zaidi ya asilimia 75 ya mbolea zote zinazoingizwa nchini na kuzalishwa na viwanda vya ndani.

Amesema, mikoa inayoongoza kwa matumizi ya mbolea katika kanda hiyo ni pamoja na Mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa, Rukwa na Katavi.

Ameongeza kuwa, kwa msimu wa kilimo 2023/2024 jumla ya wakulima 14,677 kati ya wakulima 69,073 waliosajiliwa katika mfumo wa ruzuku ikiwa ni sawa na asilimia 21.2 walinunua mbolea za ruzuku kiasi cha tani 4,097.75 zenye thamani ya ya ruzuku kiasi cha shilingi bilioni 4.5.

Amesisitiza kuwa, Serikali imekuwa ikisisitiza matumizi sahihi ya mbolea ili kuwafanya wakulima walime eneo dogo na kuvuna mazao mengi kwani ongezeko la watu duniani linapunguza eneo ambalo lingeweza kutumika kwa shughuli za kilimo.

Mwaiteleke alimalizia kwa kuuomba uongozi wa Mkoa wa Katavi na wadau wa kilimo kuunga mkono kampeni ya Kilimo ni Mbolea ili kuwaeleimisha wakulima na kuwahamasisha kuondokana na kilimo cha mazoea kisichokuwa na tija ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Mkulima Frenk kibigas mkulima wa mahindi ameishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kuweka nguvu kwenye sekta ya kilimo kwa kuweka ruzuku ya mbolea na kutoa vipimia udongo ili kuwafanya wakulima watumie mbolea sahihi kulingana na mahitaji ya udongo na hivyo kuongeza uzalishaji

Chiku Mlisho ni mkulima wa mahindi katika shamba la eka 4 kijiji cha Igalula, Mpanda Ndogo wilayani Tanganyika amefurahi kupata huduma ya kuboresha taharifa zake zitakazo muwezesha kupata mbolea ya ruzuku msimu ujao na kuongeza ekari 6 zitakazo muwezesha kupata mazao mengi yatakayo muwezesha kuinuka kiuchumi.



Post a Comment

Previous Post Next Post