NA MAGENDELA HAMISI
WATOTO 10 wenye umri wa kuwa shule wamekamatwa katika Soko la Mabibo, Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam wakijihusisha na uuzaji wa vitafunwa na mifuko huku wanaowatumikisha nao wakisakwa kwaajili ya kuwachukulia hatua za kisheria.
Hayo yamebainishwa leo, Agosti 28, 2024 jijini Dar es Salaam na Meneja wa soko hilo, Geofrey Mbwama na akafafanua kuwa mchakato huo wameufanyika leo kwa kushirikiano na maofisa wa Ustawi wa Jamii wa soko hilo na wa Manispaa ya Ubungo na operesheni hiyo itakuwa endelevu ili kudhibiti changamoto hiyo.
“Lengo la kuwakamata watoto wanaofanya biashara katika soko hili ni kuondoa tatizo la ajira kwa watoto au kuwatumikisha wa watoto ambao kimsingi wanatakiwa waendelezwe kielimu, kulindwa na kufahamu kwa nini hawapo shuleni kulingana na umri wao kuonekana kwamba wanatakiwa kuwa shule.
“Baada ya kuwahoji wamedai wanafanyabiashara hizo kutokana na ugumu wa maisha na wengine wamesema wanatafuta fedha kwa ajili ya kutafuta ada na kwetu tumeona hayo si majukumu yao, hivyo tumewapeleka katika vituo vya Kulelea Watoto Yatima kwa ajili ya kuwahifadhi na utambuzi.
“Kwa maana wazazi au walezi wanaowatumikisha watafika katika vituo hivyo kwaajili ya kuwatambua na baada ya hapo Ustawi wa Jamii watawachukulia hatua za kisheria kwa mujibu wa taratibu zao ili iwe fundisho kwa wazazi wanaowatumisha watoto na kukwepa majukumu yao ya kulinda na kuwaendeleza watoto,” amesema.
Mbwama, ameongeza kuwa operesheni hiyo itakuwa endelevu ili kuhakikisha wanaondoa tatizo la watoto kutumikishwa sokoni hapo na sheria zaidi zitaendelea kuchukuliwa kwa wazazi waowatumikisha watoto ikiwemo kupiga faini na kupiga na marufuku kufanya biashara katika soko hilo.
Pia ametoa wito kwa wazazi kwamba wasikwepe majukumu ya kulea watoto wao na waache tabia ya kuwatumikisha kufanya biashara hususan katika soko hilo.