TBS YATOA ELIMU YA KUDHIBITI SUMUKUVU URAMBO

 Na Mwandishi Wetu, Urambo


WANANCHI katika Halmashauri ya Wilaya Urambo mkoani Tabora wamepatiwa mafunzo kuhusiana na namna wanavyoweza kuepukana na sumukuvu kwenye mazao ya mahindi na karanga.

Elimu hiyo imetolewa mapema wiki hii wilayani hapa na maofisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa kushirikiana na wale wa Halmashauri ya Wilaya Urambo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Kijiji cha Songambele kilichopo Kata ya Songambele wilayani Urambo, mkoani Tabora, Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi wa TBS, Gerald Magola, alisema elimu hiyo inatarajia kufikia wananchi wa kata 15 kati ya 18 za wilaya hiyo ambazo ni zaidi ya asilimia 90.

Magola alisema wanatoa mafunzo hayo kwa sababu Serikali inatumia gharama kubwa kutibu wananchi wanaokuwa wameathirika kwa kula chakula ambacho kimechafuliwa na sumukuvu.

"Kwa hiyo lengo la mafunzo haya ni kuwaelimisha wananchi ni namna gani wanaweza kuepukana na sumukuvu katika mazao ya mahindi na karanga kwa kuweze kulima sawa sawa ili sumukuvu isiweze kuingia kwenye mazao hayo," alisema Magola.

Kwa mujibu wa Magola inafahamika kuwa sumukuvu ni moja ya sumu ambayo inaweza kuchafua mazao ya mahindi na karanga.

Aidha, alisema kuna takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinazoonesha kwamba takribani watu milioni 600 duniani huwa wanaugua kwa mwaka kwa sababu ya kula chakula ambacho kimechafuliwa na vichafuzi mbalimbali.

"Lakini pia ni takwimu hizo hizo za WHO zinaeleza kwamba takribani watu 420,000 duniani wanakufa kwa mwaka kwa sababu ya kula chakula ambacho kimechafuliwa na vichafuzi mbalimbali.

Aidha, kuna makadirio yanayoonesha kuwa katika wagonjwa 10 kuna mgonjwa mmoja anaugua kwa sababu ya kula chakula hicho. Kwa hiyo unaweza kuona ni namna gani tatizo linavyokuwa kubwa namna gani kwa sababu ya kula chakula ambacho sio salama," alisema Magola.

Alizidi kufafanua kwamba kuna takwimu zinazoonesha kwamba watoto wa miaka mitano kushuka chini duniani takribani asilimia 40 ya magonjwa yanakuwa yanawakabili wao na watoto takribani 125,000 huwa wanapoteza maisha kila mwaka kwa kula chakula ambacho kimechafuliwa na vichafuzi mbalimbali.

"Vile vile kuna takwimu zinazoonesha kuwa kuna upotevu wa nguvu kazi, lakini pia upotevu wa fedha ambao unatokana na aidha kutibu wagonjwa ambao wanakuwa wameathirika kutokana na ulaji wa chakula kisichikuwa salama, lakini pia kuna gharama kubwa Serikali inakuwa inaingia kwa ajili ya kutenga fedha kununua dawa na vifaa tiba ili kuwahudumia wagonjwa," alifafanua Magola.

Kutokana na takwimu na madhara hayo, Magola alisema kwamba Serikali inatamani kuzuia athari hizo ili kuhakikisha watu wanakuwa na afya nzuri hatimaye waweze kushiriki kwenye majukumu yao mbalimbali yatakayowawezesha kujiingiza kipato chao, lakini pia kuongeza tija kwa Serikali.

"Hivyo tumekuja wilaya ya Urambo kwa ajili ya kutoa mafunzo haya kuanzia tarehe 26 hadi Tarehe 30 Agosti tumekwisha kutoa mafunzo katika kata 15 kati ya 18 za wilaya hiyo sawa na asilimia zaidi ya 90”, alisema Magola na kuongeza;

"Elimu hii itawawezesha pia kuweza kuvuna sawa sawa na kuchakataka mazao hayo inavyotakiwa ili kuwa na kizazi salama kinachotumia mazao haya."

Alisema wananchi wa Wilaya ya Urambo ni miongoni mwa walengwa wa elimu hiyo kwa sababu ni miongoni mwa wazalishaji wa mazao hayo hasa kwa kuzingatia kuwa wote tunafahamu kuwa chakula hakizalishwi mijini, isipokuwa inawezekana mijini kinachakatwa.

"Kile chakula halisi kinatoka kijijini kwa hiyo ndiyo maana Serikali imeona kuna umuhimu mkubwa wa kwenda vijijini kuhakikisha wananchi wanafikiwa elimu, kwani ndiyo wazalishaji wakubwa wa vyakula," alisema Magola na kusisitiza kwamba wananchi hao wakipata elimu hiyo tutaweza kupata chakula ambacho ni salama.




Post a Comment

Previous Post Next Post