Na Mwandishi Wetu ,Ngorongoro
Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) inapenda kutoa taarifa kwa umma kuwa zoezi la kuelimisha na kuhamasisha wananchi wanaoishi katika hifadhi ya Ngorongoro kuhama kwa hiyari linaendelea ikiwa ni hatua ya kulinda hifadhi hiyo na kuboresha ustawi wa maisha ya wananchi wa Ngorongoro.
Zoezi hilo linaloendelea katika vijiji mbalimbali ndani ya hifadhi linalenga kupunguza shughuli za kibinadamu kutokana na ongezeko kubwa la watu na mifugo katika eneo la hifadhi lenye ukubwa wa kilomita za mraba 8,292 pekee.
Kutokana na sheria za uhifadhi zinazozuia baadhi ya shughuili za kiuchumi kama Kilimo, kuweka umeme, uhuru wa kutembea usiku kutokana na uwepo wa Wanyama wakali pamoja na masharti mengine hivyo Serikali iliamua kutafuta maeneo nje ya hifadhi ili kuboresha maisha ya wananchi wa Ngorongoro na kulinda hifadhi.
Dhamira ya Serikali kuboresha Maisha ya wananchi ni tofauti na maelezo ya upotoshaji yaliyoandikwa na gazeti la Mwanahalisi toleo namba 471 lililoandika kuwa zoezi la kuhamisha wananchi kwa hiari linalenga kutaka kukabidhi sehemu ya eneo hilo kwa kampuni ya uwindaji ya `Otterlo Business Corporation (OBC). Kampuni hii iliyotajwa haipo katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro isipokuwa imewekeza katika eneo la Pori la akiba la Pololeti ambapo pia kuna wawekezaji wengine ambao kwa pamoja wapo kwa mujibu wa sheria za nchi.
Mamlaka inawaomba wananchi wote kupuuza taarifa ambazo hazina ukweli na zenye lengo la kuupotosha umma ama kuwachonganisha na serikali yao kuhusiana na zoezi zima la wananchi kuhama kwa hiyari kutoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro. Serikali inaendelea kuboresha huduma za jamii kwa wananchi waliopo ndani ya hifadhi ya Ngoromgoro pamoja na kujenga na kuboresha huduma za kijamii katika maeneo mengine nje ya hifadhi ambayo wananchi wanahamia.
Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro itaendelea kutumia njia mbalimbali za mawasiliano, majadiliano, ushirikishwaji na kuwaelimisha wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi ili kwa hiari yao wenyewe waweze kuhama huku serikali katika utekelezaji wake ikizingatia sheria na taratibu zote pamoja na kulinda misingi ya haki za binadamu.