REA KUPELEKA UMEME VIJIJI 151 AMBAVYO HAVIJAFIKIWA NA TANESCO.

 WAKALA wa Nishati Vijijini (REA), imesema wanaendelea kusambaza nishati vijijini ambapo vijiji 151 ambavyo havijafungwa umeme Tanzania Bara, vinatarajiwa kukamilika kabla ya Septemba mwaka huu huku Vijiji vilivyosalia vikiwa kwa wakandarasi kwaajili ya kukamilishwa ikiwa ni kati ya vijiji 12,318 vilivyopo nchini na kati ya hivyo 12,167 zimeshafungwa umeme.


Hayo yamesemwa Julai 13,2024 Jijini Dar es Salaam na Mhandisi Mchunguzi wa REA, Jones Oloto,wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara(Sabasaba).

Amesema baada ya kukamilisha kufunga vijiji vilivyobaki watabakisha vitongoji 32,427 vinavyotakiwa kufikiwa na umeme kati ya 64,359 vilivyopo nchini.

Oloto amesema katika mpango wa miaka mitano vitongoji 20,000 vinatarajiwa kuwekewa umeme.

Amesema wataanza na vitongoji 4,000 kila mwaka kwa kuanzia mwaka mpya wa fedha 2024/25 kumaliza katika kipindi cha miaka hiyo mitano ambapo vitabaki vitongoji zaidi ya 8,000 ambavyo vitamalizwa kwa kipindi cha miaka mingine miwili na nusu.

“Baada ya kumaliza tutahamia hatua ya nyumba kwa nyumba. Kule vijijini kuna nyumba nyingine zinakuwa mbali na miundombinu lakini kuna nyumba mpya zinaibuka zinatakiwa kufungwa umeme pamoja na taasisi za afya ambazo zinajengwa,” amesema.

Ameongeza kuwa, kuna miradi maalum ya kupita kwenye taasisi za afya, elimu, migodi, vituo vya polisi na mahakama ndogo ambao idadi yake ipo na wataendelea kutoa huduma.

“Kila sekta tunayogusa lengo ni kuinua wananchi kiuchumi kwasababu umeme unarahisisha shughuli za wananchi kiuchumi,” amesema.

Post a Comment

Previous Post Next Post