DKT ABBAS AIPONGEZA SUMA -JKT KWA HATUA NZURI YA UJENZI WA NYUMBA 2500 MSOMERA.


 Na Mwandishin wetu Handeni.

Katibu Mkuu wa wizara ya Maliasili na Utalii Dkt Hassan Abbasi amelipongeza Jeshi la Kujenga Taifa kupitia kampuni yake ya SUMA -JKT kwa kufikia zaidi ya asilimia 90 kukamilisha ujenzi wa nyumba 2,500 zinazojengwa katika Kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoani Tanga.

Dkt Abbasi ametoa kauli hiyo katika ziara aliyoifanya Kijijini hapo tarehe 8 Julai, 2024 na kusema kazi iliyofanywa na jeshi hilo ni kubwa na ya kizalendo hivyo zoezi lililobaki sasa ni kuendelea kuelimisha, kuhamasisha na kuhamisha wananchi wanaoendelea kujiandikisha kuhama kwa hiyari katika eneo la tarafa ya Ngorongoro.

Amesema kuwa ujenzi wa nyumba hizo unaenda sambamba na ujenzi wa miundombinu mingine ya huduma za kijamii ambapo wizara za kisekta zimekuwa zikiendelea kujenga miundo mbinu hiyo ikiwemo shule,usambazaji wa umeme,maji ,mawasiliano na huduma zote za msingi katika Kijiji hicho.

Katibu mkuu huyo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan kutokana na maono yake kaatika utekelezaji wa mradi huo ambao kukamilika kwake kutatimiza utekelezaji wa malengo ya serikali ya kuhakikisha kila mtanzania anakuwa na maisha bora.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Handeni mheshimiwa Albert Msando amemshukuru Dkt Abbasi kwa ziara hiyo na kusema kuwa itaongeza ari kwa wizara nyingine za kisekta kuongeza kasi katika ukamilishaji wa miradi yote muhimu na hivyo kuifanya Msomera kuwa Kijiji cha mfano.

Mheshimiwa Msando amesema kuwa uendelevu wa mradi huo unaondoa propaganda za watu wachache kwamba wananchi wanaohamishwa kutoka Ngorongoro kwenda katika Kijiji hicho wanaondolewa kwa nguvu na kutelekezwa jambo ambalo halina ukweli wowote.

Akizungumzia kuhusu suala la kuhamisha watu kwa hiyari kutoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro Kamishna wa Mamlaka ya Uhifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Dkt.Elirehema Doriye amsema kukamilika kwa nyumba hizo kunaongeza chachu ya mamlaka kuendelea kuhamasisha na kuhamisha wananchi.

Mapema Kamanda wa Operesheni wa Ujenzi wa nyumba hizo kanali Sadiki Mihayo alimweleza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt.Hassan Abbasi kwamba ujenzi wa nyumba zote 2500 upo hatua za mwisho kukamilika na sasa wanajiandaa kuhamia katika wilaya kijiji cha Kitwai wilaya ya Simanjiro na kijiji cha Saunyi wilaya ya Kilindi kuendelea na ujenzi wa nyumba zilizobaki kulingana na mpango kazi waliojiwekea.  

Post a Comment

Previous Post Next Post