WAZIRI MCHENGERWA ATUA KWENYE MAPOROMOKO YA MPANGA KIPENGERE, AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI, WAGENI

 


Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa wito kwa watanzania kujitokeza kutembelea maeneo ya utalii wa maporomoko ya maji ambayo yana historia kubwa ya utamaduni wa nchi yetu pia ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kufungamanisha utalii na utamaduni wa Taifa la Tanzania.

Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo alipotembelea leo maporomoko ya Mpanga Kipengere yaliyopo katika mpaka wa mkoa wa Mbeya na Njombe na kukagua shughuli mbalimbali za utalii na miundumbinu iliyojengwa na  Mamlaka ya Wanyamapori Nchini (TAWA) kwa ajili ya kuhudumia wageni mbalimbali wanaotembelea  maeneo hayo.


“Napenda kutoa wito kwa viongozi wa kuchaguliwa na wananchi na kuteuliwa kuwahimiza wananchi kuja  kutembelea maeneo haya  ili kuona urithi wa hazina ya utalii na utamaduni ambao haupatikani sehemu yoyote duniani isipokuwa katika maeneo hayo.”amefafanua Mhe. Mchengerwa

Amewataka watanzania kuchangamkia fursa ya uwekezaji kwenye maeneo haya ambapo amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kutangaza maeneo yote yenye fursa za uwekezaji  ili watu wenye  uwezo wa kuwekeza waweze kuwekeza  hatimaye  kuliingizia taifa  mapato.

Akizungumzia kuhusu maboresho ambayo Serikali inakwenda kufanya kwenye  maporomoko ya Mpanga Kipengere kwa sasa ni pamoja  na kujenga  miundombinu ya kupumzikia wageni wageni, kuweka makasia na zip line.

Ameyataja maporomoko mengine ambayo ni sehemu ya Mpanga Kipengere kuwa ni pamoja na Kimani, Nyaugenge, Ikovo, Kipengere, Lyamakunohila na Nyaluliva ambayo  kila moja  lina aina ya utalii wa kipekee.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi Joas Makwati wa Mpanga Kipengere amefafanua  kuwa mbali ya kuwa eneo  ni maarufu kwa  maporomoko  pia  lina maua  ya kipekee, safu za milima  na Wanyama  wa porini kama Mbuzi Mawe na toe.

Makwati amesema eneo hili ni miongoni mwa eneo mkakati kwa utalii nchini  kutokana  na eneo lililopo kijiografia  ambapo amesema  endapo juhudi za makusudi za kuleta  wanyama  zikifanyika zitasaidia kuwavutia wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani kutembelea.

Aidha, amefafanua  kuwa awali eneo hili  lilikuwa na Wanyama wengi chini ya umiliki wa vijiji ambapo uwindaji haramu ulitamalaki  hivyo  kumalizika kwa Wanyama waliokuwepo.

Post a Comment

Previous Post Next Post