JAJI KIONGOZI AONGOZA SHEREHE YA KUWAAGA KITAALUMA MAJAJI WASTAAFU

 Na Mary Gwera, Mahakama

JAJI Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani ameongoza sherehe ya kuwaaga kitaaluma Majaji watatu wastaafu wa Mahakama hiyo ambapo amesema kwamba, Mhimili huo utaendelea kusimamia haki katika utendaji kazi na kuwaomba wananchi kuendelea kuwa na imani na chombo hicho.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo tarehe 04 Mei, 2023 mara baada ya kuhitimisha zoezi la kuongoza sherehe hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam, Mhe. Siyani amesema kuwa ni wajibu wa Majaji na watumishi wote wa Mahakama kuhakikisha kwamba wanaendelea kujenga imani ya wananchi dhidi ya Mahakama.

“Wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi na Mahakama, hivyo niwakumbushe wananchi kuendelea kutumia Mahakama zote kuanzia ngazi ya Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama ya Rufani kwakuwa ndipo haki inapopatikana,” amesema Jaji Kiongozi.

Mhe. Siyani amesema kwamba, wananchi wanapokosa imani kwa Mahakama maana yake hawatatumia chombo hicho na hivyo kutakuwa na ongezeko la vitendo vya uhalifu vitakavyohatarisha amani ya nchi.

Akizungumzia kustaafu kwa Majaji hao ambao ni Mhe. Beatrice Rhoda Mutungi, Mhe. Sekela Cyril Moshi na Mhe. John Mgetta, Jaji Kiongozi amesema kuwa watakumbukwa kwa uzoefu na umahiri wao katika kuendesha gurudumu la utoaji haki nchini.


“Kustaafu kwa Majaji hawa waliokuwa na uzoefu wa kutosha ni dhahiri kuwa kumeacha pengo, hivyo nitoe rai kwa Majaji wanaobaki kuchukua mazuri yote ambayo yameachwa na Majaji hawa ili kuendelea kuwahudumia vema wananchi,” ameeleza Mhe. Siyani.


Wakizungumza katika sherehe hiyo ya kitaaluma, Majaji wastaafu walioagwa wametoa rai kwa watumishi wa Mahakama kuimarisha ushirikiano katika kazi, kutokuwa na upendeleo, kufanya kazi kwa bidii na kuendeleza matumizi ya TEHAMA.


Katika sherehe hiyo maalum ya kitaaluma Jaji Kiongozi aliongoza jopo lenye jumla ya Majaji 24 wa Mahakama Kuu na vilevile imehudhuriwa na pia baadhi ya watumishi na Viongozi wa Mahakama ambao ni pamoja na Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Martin Chuma. Kadhalika imehudhuriwa na ndugu, jamaa na marafiki wa Majaji wastaafu.


Wadau waliohudhuria katika sherehe hiyo ni pamoja na Mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Makamu wa Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS).


Zoezi la kuwaaga kitaaluma Majaji wastaafu linafanyika kwa mujibu wa Waraka Na. 1 wa Mwaka 2006 wa Jaji Mkuu.

Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji watatu wastaafu walioagwa leo pamoja na baadhi ya Majaji wa Mahakama hiyo walioshiriki katika sherehe ya kuagwa kitaaluma kwa Majaji wastaafu iliyofanyika leo tarehe 04 Mei, 2023 katika ukumbi namba moja (1) wa Mahakama Kuu Dar es Salaam. Majaji wastaafu walioagwa ni pamoja na Mhe. Beatrice Rhoda Mutungi (wa kwanza kushoto kwa Jaji Kiongozi), Mhe. Sekela Cyril Moshi (wa pili kushoto) na Mhe. John Mgetta (wa kwanza kushoto).

Post a Comment

Previous Post Next Post