TRA YAFANYA SEMINA NA WAMILIKI, WATUMIAJI WA MAGHALA YA KUHIFADHIA BIDHAA

 








 KAMISHNA wa Kodi za Ndani Herbert Kabyemela amewakumbusha wamiliki na watumiaji maghala ya kuhifadhia bidhaa (Storage Facilities) kusajili sehemu hizo kwa Kamishna Mkuu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

 Amefafanua kuwa mchakato wa kusajili maghala huko kisheria kulingana na Sheria ya Usimamizi wa Kodi nchini na ni lazima kila mmiliki au mtumiaji aufuate,  aliyasema hayo  leo Mei 10, 2023 katika semina iliyofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Upanga jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake Mwezeshaji wa semina hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Mlipakodi,  Stephen Kauzeni, amesema Sheria ya Fedha ya Mwaka 2022 kifungu cha 45A chini ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi sura ya 438, inawataka wamiliki au watumiaji wa maeneo ya kuhifadhia bidhaa kuyasajili kwa Kamishna Mkuu.

Aliongeza kuwa kifungu hicho kwa mujibu wa taratibu za kisheria kimeanza kutumika rasmi tangu Julai Mosi, 2022 hali inayotoa fursa kwa mmiliki au mtumiaji wa ghala la kuhifadhia bidhaa kuifuata bila kusukumwa.

Katika hatua nyingine wafanyabiashara ambao wameudhuria semina hiyo wameipongeza na kuishukuru TRA, kutokana na kwamba warsha hiyo imewapa uelewa mkubwa kuhusu mabadiliko hayo ya sheria na wameahidi kuitelekeza kwa vitendo ili kutimiza wajibu wao kisheria kwa kusajili maghala yao kwa wakati.

TRA kupitia Idara ya  Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, imekuwa na utaratibu wa kuendesha semina mbalimbali zinazohusu masuala ya kikodi ili kuwajengea uelewa walipakodi.

Post a Comment

Previous Post Next Post