DKT. ABBAS AITAKA MAKUMBUSHO YA TAIFA KUIMARISHA UHIFADHI NA UTANGAZAJI.

 

Na Joyce Mkinga

Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas ameitaka Makumbusho ya Taifa la Tanzania kuimarisha uhifadhi na utangazaji wa makumbusho na malikale ili kuhakikisha zinajulikana kitaifa na kimataifa.

Dkt. Abbas ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam, alipokutana na menejimenti ya Makumbusho ya Taifa kwa lengo la kupata uelewa wa pamoja juu ya uhifadhi na Utangazaji wa Makumbusho na Malikale nchini.

Amesema kazi ya uhifadhi katika makumbusho na malikale ni kazi ya kiroho inayomkumbusha binadamu alikotoka na anakokwenda kwa faida ya kizazi cha sasa na vijavyo, hivyo, suala la uhifadhi endelevu na utangazaji ni muhimu.

“Mwelekeo wa Wizara yetu kwa kipindi hiki na kijacho ni uhifadhi na utangazaji wa makumbusho na malikale ili watu wajue tunachosimamia,” alisema Dkt Abbas.

Aidha, ameitaka Makumbusho ya Taifa nchini pale inapotafuta rasilimali na watalaam mbalimbali katika uendeshaji wa makumbusho na malikale lazima wazingatie masuala muhimu ya uhifadhi na utangazaji.

Licha ya Kuipongeza Makumbusho ya Taifa kwa uhifadhi wa urithi wa Historia, Dkt. Abbas ameitaka Taasisi hiyo Kufanya kazi kwa bidii na kuongeza ubunifu katika utangazaji hasa kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii katika kutangaza fursa za utalii zinazopatikana katika Makumbusho na Malikale.

Post a Comment

Previous Post Next Post