WATAKIWA KUTEKELEZA KANUNI ZA WAMILIKI MANUFAA



Wamiliki wa Kampuni wametakiwa kutekeleza  Kanuni za  Wamiliki Manufaa wa Kampuni ili kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

Rai hiyo imetolewa  na Mkuu wa mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera, tarehe 29 Machi, 2023 katika hoteli ya Royal Tughimbe  jijini Mbeya, wakati akifungua Warsha  kuhusu  utekelezaji wa kanuni za  Wamiliki Manufaa iliyowashirikisha Mawakili wa Kujitegemea, Washauri wa Biashara, Wafanyabiashara Watumishi wa Benki, Wahasibu na Wakaguzi wa Mahesabu,  ambazo zinawataka kuwasilisha taarifa za Wamiliki Manufaa wa Kampuni kwa Msajili wa Makampuni.

"Nimefahamishwa kuwa Kampuni nyingi bado hazijawasilisha taarifa hizo kwa Msajili wa Makampuni, inawezekana kuna changamoto katika  uandaaji wa taarifa hizo na namna za kuziwasilisha Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni  (BRELA), hivyo ni vyema mkatumia fursa hii kutatua changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa uwasilishaji wa taarifa hizi ambazo ni muhimu kwa mujibu wa sheria," amefafanua Mhe. Homera.

Awali akizungumza  kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa, Mkuu wa Sehemu ya Kampuni Bw. Isdor Nkindi amesema, mkoa wa Mbeya ni kati ya mikoa mitano iliyochaguliwa kutekeleza program hiyo kutokana na takwimu nzuri ya mzunguko wa biashara na mwamko uliopo wa urasimishaji biashara. 

Bw. Nkindi amesema BRELA pamoja na majadiliano na wadau wa biashara kuhusu utekelezaji wa kanuni za Umiliki Manufaa,  katika warsha hiyo washiriki watapatiwa nyenzo za kutumia wakati wa kuainisha Wamiliki Manufaa katika kampuni wanazozishauri na wanazoziendesha.

Sheria ya  Bunge la Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania kupitia Muswada wa  Sheria ya Fedha, ilipitisha marekebisho ya Sheria ya Kampuni Sura ya 212 kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa taarifa za Wamiliki Manufaa ambazo ni muhimu katika kuboresha mazingira ya uwekezaji, kikodi pamoja na kudhibiti utakatishaji wa Fedha haramu na ufadhili wa vitendo vya ugaidi.

Vilevile, mwaka 2021 Waziri mwenye dharna alipitisha Kanuni za Umiliki Manufaa katika kampuni na kuanza kutumika rasmi mwaka 2022.

Maafisa wa BRELA  watakuwepo mkoani Mbeya kwa siku mbili kutekeleza jukumu hilo.

Post a Comment

Previous Post Next Post