WAZIRI MCHENGERWA AWATAKA WASIMAMIZI WA MIRADI YA (REGROW) KUONDOA UKIRITIMBA

 

Mhe. Mchengerwa atema cheche kwenye utiaji saini wa mikataba ya REGROW ya bilioni 157, asisitiza REGROW utafungua utalii na uchumi wa mikoa ya kusini.

…………………

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa  amewataka watekelezaji wote wa Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii kusini (REGROW)  kuondoa ukiritimba wakati wa kutekeleza mradi huu ili kukuza na kutangaza mazao mapya ya utalii katika mikoa ya kusini mwa Tanzania vinginevyo hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobainika kufanya uzembe au kuuhujumu mradi huo.

Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Aprili 16, 2023 jijini Arusha wakati akitoa hotuba yake kwenye hafla ya utiaji saini mikataba nane ya ujenzi wa miundombinu yenye thamani ya shilingi bilioni 157.29 chini ya mradi wa kuboresha usimamizi wa Maliasili na kukuza utalii kusini mwa Tanzania

“Wanaopaswa kwenda kusimamia lazima waende wakasimamie na watendaji ambao watabainika kutofanya vizuri watachukuliwa hatua, dhamira ya serikali ni kuhakikisha kuwa tunafanya vizuri ili twende tukapate fedha zaidi katika awamu ya pili.” Amesisitiza Mhe. Mchengerwa

Waziri Mchengerwa amewataka wakandarasi wote waliosaini mikataba hiyo kutumia vizuri muda waliopewa kwa kufanya kazi nzuri katika muda mfupi na kwamba wasitarajie kuongezewa muda.

Mikataba iliyosainiwa imegawanyika katika makundi mawili; mikataba minne ya ujenzi wa majengo pamoja na mikataba minne ya ujenzi wa viwanja vya ndege ambayo itatekelezwa katika hifadhi nne za Ruaha, Mikumi Udzungwa na Nyerere na Msitu wa Asili wa Kilombero chini ya TFS .

Akifafanua zaidi amesema kwenye mikataba ya ujenzi wa viwanja inatarajiwa viwanja sita vya ndege kujengwa ambapo viwanja vitatu vya ndege vitajengwa hifadhi ya Ruaha , viwanja viwili hifadhi ya Mikumi na hifadhi ya Nyerere kitajengwa kiwanja kimoja cha ndege.Aidha amesema katika hifadhi ya Udzungwa kutajengwa njia ya juu ya watalii ambayo inakadiriwa kuwa na kilomita moja ambayo inatarajiwa kuwa miongoni mwa njia ndefu zaidi Afrika Mashariki na hata kusini mwa Afrika itakapokamilika.

Post a Comment

Previous Post Next Post