VYUO TANZANIA, AFRIKA KUSINI KUZALISHA WATAALAM VIWANGO VYA “ROYAL TOUR” SEKTA YA UTALII

 


Katika kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha sekta ya utalii nchini hasa baada ya Rais kushiriki filamu ya “Tanzania; The Royal Tour,” sasa wataalamu zaidi wa Tanzania watanufaika na mafunzo ili kuboresha uwezo wao kuendana na viwango vya kisasa.

Hayo ni sehemu ya makubaliano ya awali yaliyosainiwa leo Machi 14, 2023 jijini Pretoria, Afrika Kusini, kati ya Chuo cha Taifa cha Utalii cha Tanzania (NCT) kilichowakilishwa na Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Florian Mtey na Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Tshwane cha Afrika Kusini ambacho kimewakilishwa na Dkt. Edgar Nesamvuni.

Utiaji saini wa mkubaliano hayo umeshuhudiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi akimwakilisha Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa, na pia kuhudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Afrika ya Kusini Meja Jenerali (Mstaafu), Gaudence Milanzi kwenye ofisi za Ubalozi wa Tanzania Pretoria.

Kupitia vyuo hivyo, nchi hizo mbili zitashirikiana katika kuzalisha wataalamu wa biashara ya utalii, kuboresha ukarimu na kubadilishana uzoefu na wataalamu wa mafunzo katika nyanja mbalimbali za utalii.

Akizungumza baada ya hafla ya utiaji saini Katibu Mkuu Dkt. Abbasi amesema makubaliano hayo yatasaidia kuboresha uwezo wa wafanyakazi wetu kwenye sekta ya utalii ili waendane na matokeo chanya yanayoletwa nchini na filamu ya “Royal Tour.”

“Vyuo vyetu hivi viwili vitakuwa chachu ya kuboresha utalii nchini Tanzania na inakuja wakati ambapo Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kutangaza utalii nchini kwa kushiriki filamu ya Royal Tour”. Amesema Dkt. Abbasi.

Naye Balozi Milanzi aliyeshiriki kuratibu mkataba huo tangu mwanzo, amewashukuru viongozi wa Vyuo hivyo Dkt. Mtey wa Chuo cha Taifa cha Utalii na Dkt. Edgar wa Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Tshwane kwa kukamilisha mazungumzo hayo.

Chuo cha Taifa cha Utalii, Tanzania kinakuwa Chuo cha kwanza Afrika kuingia makubaliano na Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Tshwane cha Afrika ya Kusini ambacho ni cha pili kwa ukubwa Afrika chenye jumla ya wanafunzi elfu sitini (60,000).

Hafla hiyo imehudhuriwa pia na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Bw. Kheri Mahimbali, pamoja na viongozi wengine wa Wizara na Ubalozi.   

Post a Comment

Previous Post Next Post