TTB YAAGIZWA KWENDA KIMATAIFA, KIDIGITI KUITANGAZA TANZANIA

 


Na John Mapepele

Katika mwendelezo wa kujifunza na kujipanga, leo Februari 21, 2023, Waziri wa Maliasili Mhe. Mohamed Mchengerwa na Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi, wametembelea Bodi ya Utalii (TTB) jijini Dar es Salaam; chombo muhimu kilichopewa dhamana na dhima ya kutangaza na kufanya uraghibishaji wa sekta ya utalii ndani na nje ya nchi.

“Hapa lazima tukiri yapo yaliyofanyika lakini bado tuna kazi kubwa kuutangaza utalii wetu ndani na nje ya nchi. Kazi ipo hapa. Nataka mje na mikakati zaidi na hasa kutumia teknolojia lakini pia tuwe na slogan moja inayoeleweka kuliko sasa kila mtu ana yake ili kuutangaza utalii kimataifa zaidi,” amesema Mhe. Mchengerwa.

“Mnaweza kuwa mmefanya mengi lakini Watanzania bado hawajaona kama mmefika pakubwa sana. Tuendako tutalala pamoja hapa kuja na mikakati kabambe kuendeleza pale Mhe Rais Mama Samia alipoishia katika Royal Tour,” aliongeza Dkt. Abbasi.

Ametoa maelekezo kadhaa ya kuboresha sekta ambapo ametoa miezi miwili ya kufanya mapinduzi katika sekta zote hususan katika eneo la uhifadhi wa raslimali za kutangaza Utalii ndani na nje ya Tanzania.

Baadhi ya mambo ambayo amesisitiza ni pamoja na kufufua Kitengo cha utafiti na maendeleo, kuwa na mkakati wa kukuza utalii kimataifa, kutambua vivutio vya utalii na kuendeleza makumbusho.

Aidha amesema ni muhimu kuendelea kujitangaza kwa kutumia ofisi za balozi zetu katika nchi mbalimbali duniani.

Amepongeza baadhi ya balozi kama Saudi Arabia na China ambazo zimekuwa na mikakati ya kuleta watalii nchini.

Aidha, amesema ni vizuri kuendelea kutumia mashirika makubwa ya ndege, timu kubwa za michezo duniani kuvitangaza vivutio vya utalii.

Pia, ameitaka Menejimenti na taasisi hiyo kuandaa app ambayo itawezesha kutoa tafsiri ya lugha mbalimbali ambazo zitasaidia wageni wanaokuja nchini.

Amehoji ni kwa nini wageni wakija mara moja nchini hawarudi tena wakati Tanzania ina utulivu wa kisasa na kuna utashi wa viongozi wakuu wa nchi.

Amewataka pia kushirikiana na wadau mbalimbali wakati wa kutekeleza mikakati ya kuitangaza Tanzania.

Wakati huohuo akiwa hapo Mhe. Mchengerwa amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uholanzi Mhe. Wiebe de Boer jinsi ya kufanya mashirikano kwenye utalii.   

Post a Comment

Previous Post Next Post