TRA YABORESHA MFUMO WA KODI WA KIELEKTRONIKI


                         ........................
NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA  ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Kodi Ilala na Kariakoo kwa kushirikiana na Assad Associates, wameendesha semina kuhusu mfumo wa Kodi wa Kielektroniki ambao umeboreshwa.
Mfumo huo mpya ambao umeboreshwa utawezesha kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili walipa kodi hususan wanaowasilisha ritani zao kwa njia ya mtandao.

Hayo yamebainishwa leo, jijini Dar es Salaam na Kaimu Kamishna wa Kodi za Ndani, Michael Mhoja wakati akifungua semina hiyo na kuwaomba wadau na watumiaji wa mfumo huo, kuutumia kikamilifu ili kuokoa muda katika shughuli zao.

Pia, Mhoja alibainisha kuwa kupitia mfumo huo mpya ambao umefanyiwa maboresho wadau hao wataweza kujihudumia na hakutakuwa na haja ya kufika katika ofisi za TRA, kwa mahitaji wanayoweza kuyatatua wenyewe kupitia mfumo huo.

"Kwa sasa hakuna haja tena ya kutembelea ofisi za TRA kwa mambo ambayo unaweza kuyafanya mwenyewe huku ukiwa unaendelea na shughuli zako kupitia mfumo huu", amesema.

 Mhoja, katika hatua nyingine amewasisitiza wafanyabiashara na wanunuzi kutoa na kudai risiri sahihi za EFD kwenye mauzo na manunuzi wanayofanya kwa wakati wote wa shughuli zao. 

"Kumekuwa na tabia ya baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kutoa risiti zenye fedha pungufu kulinganisha na bidhaa wanazouza, hivyo yeyote akibainika kufanya udanganyifu huo sheria kali zitachukuliwa zidi yake" , amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo, amewapongeza wadau hasa wafanyabiashara ambao wameweza kuvumilia kipindi chote ambacho walipata changamoto za kimtandao wakati wa kuwasilisha ritani zao.

 "Najua kuna baadhi yenu mlipata changamoto kuwasilisha ritani hasa tarehe za mwisho za kuwasilisha ritani hizo lakini niwashukuru kwa uvumilivu wenu", amesema.

 Aidha, Kayombo amewataka wafanyabiashara na watumiaji wa mfumo huo ulioboreshwa, wasisite kuwasiliana na TRA  endapo watapata changamoto yoyote kwenye kutumia mfumo huo.

Wakati huo huo, wafanyabiashara na watumiaji wa mfumo huo wameipongeza, TRA kwa kuweza kuboresha mfumo huo kwani utaondoa changamoto na kero walizokuwa wakizipata hapo awali.
MWISHO

Post a Comment

Previous Post Next Post