Na Mwandishi wetu-MOI
Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) zimeanza kutoa mafunzo maalum ya upasuaji wa vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo kwa mbinu za kisasa kwa madaktari bingwa waliohitimu katika chuo hicho ambapo wagonjwa 4 wamefanyiwa upasuaji huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface amesema mafunzo hayo yanaongozwa na Mkufunzi maalum kutoka hospitali ya St. Luke`s, Ugiriki kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutoa matibabu ya kibobezi.
“Mafunzo haya ni endelevu ambapo wataalam wetu watafundishwa upasuaji wa vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo kwa mbinu za kisasa ambapo mpaka sasa wagonjwa wanne kati ya saba waliopangwa wameshafanyiwa upasuaji huo” amesema Dkt. Boniface
Aidha, Dkt. Boniface ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya kwani zaidi ya Millioni 50 zimeokolewa kama wagonjwa hao wangetibiwa nje ya nchi.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu Dkt. Nicephorus Rutabasibwa amesema Madaktari bingwa watatu wa MOI waliohitimu Chuo cha MUHAS watafundishwa mbinu za kisasa za na za kibobezi zakutibu magonjwa ya mishipa ya damu kwenye ubongo.
“Mafunzo haya yamegawanyika katika sehemu nne ambapo tunalengo la kuwafanyia wagonjwa 40 katika kipindi cha mwaka mmoja kwa ajili ya kuwajengea uwezo wataalam wetu ili baadae wawafundishe wenzao waliopo katika hospitali mbalimbali nchini” amesema Dkt. Rutabasibwa
Naye, Mtaalamu Bingwa Mbobezi wa Mishipa ya damu kwenye Ubongo kutoka hospitali ya St. Luke`s kutoka Ugiriki Prof. Athanasios Petridis amesema anafuraha kubwa kuwa MOI na kutoa mafunzo ya kibobezi ya upasuaji wa kuzibua vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo na baada ya mafunzo hayo wataalam hao watakuwa na uwezo mkubwa wa kufanya upasuaji huo.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa Ubongo Dkt. John Michael Mtei ameushukuru uongozi wa Taasisi ya MOI kwa mafunzo hayo kwani yamewajengea uwezo wa kutibu magonjwa ya mishipa ya damu kwenye ubongo .