Mhe. Mchengerwa atatua mgogoro wa mwekezaji na wananchi, wananchi wampongeza Rais Samia.

Na John Mapepele

Wananchi wa eneo la Nyanda  na Utunge wilayani Rufiji wamemshukuru Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mbunge wa Rufiji na MNEC wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Mohamed Mchengerwa kwa kutatua mgogoro wa muda mrefu baina ya mwekezaji wa mradi wa uzalishaji wa sukari na wananchi wa maeneo hayo.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa wananchi na Mhe. Mchengerwa leo, Januari 22,2023 kwenye eneo la Nyanda, Mwenyekiti Mstaafu wa Kijiji hicho, Amir Omary Magulu amempongeza Mhe. Mchengerwa kwa busara na  jitihada  zake  za kuumaliza  mgogoro huo ambao ulikuwa sugu kwa muda mrefu sasa.

Amesema mgogoro huo baina ya mwekezaji huyo ambaye ni Lake Agro  unatokana na ukiukwaji wa makubaliano ya awali  ya  kupewa eneo la uwekezaji na  kutopata taarifa sahihi za uwekezaji.

Akitoa suluhisho la mgogoro hilo, Mhe. Mchengerwa ameuomba uongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Rufiji kuja kwa wananchi  pamoja na mwekezaji ili kujadili  kwa uwazi uwekezaji huo ili kurekebisha tofauti hizo na kuendelea kutekeleza mradi huo mkubwa wa pili nchini wa uzalishaji wa sukari.

Amefafanua kuwa changamoto iliyopo ni mawasiliano hafifu ya mwekezaji kwa wananchi ambayo yamesababisha wananchi kutoelewa kinachoendelea katika mradi huo.

Ameongeza kuwa, uongozi wa Wilaya na Halmashauri usimamie  makubaliano yaliyofikiwa awali na kwamba mwekezaji asipewe eneo la pili alilolitaka  hadi akae na kukubaliliana na wananchi wa maeneo  hayo.   

Aidha, amesema  Serikali inayoongozwa  na Rais Samia Suluhu Hassan tayari imeshatoa fedha nyingi kwa ajili ya kusaidia wananchi wa Tanzania ikiwa ni pamoja na wanarufiji ambapo amesema  kwa upande wa Rufiji   tayari Serikali imetenga Bilioni 46 kujenga barabara  ya Nyamwage  hadi Utete pia kutoka Ikwiriri hadi Mkongo. 

Kwa upande wao, Rashidi Omari Goboleni na Asha Juma Mbonde wamemshukuru na kumpongeza Mhe. Mchengerwa kwa  maelekezo yake ya kumaliza  mgogoro  huo huku wakisifu jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikaliza kuwaletea maendeleo.

“Tumefurahishwa sana na ujio wa Mbunge wetu leo na kumaliza kabisa mgogoro huu, natumaini sasa tutapiga  hatua. Asante sana  mama Samia  kwa kutushika  mkono” ameongeza  Nyamkiu Mohamed Mkiu mkazi wa Kijiji cha Utunge


Post a Comment

Previous Post Next Post