BRELA YAWANOA WAFANYABIASHARA ELIMU YA MILIKI UBUNIFU







 NA MWANDISHI WETU

WAFANYABIASHARA nchini wametakiwa kulinda na kutumia vema alama zao za biashara na Huduma ili kulinda uchumi na kuondoa migogoro baina yao na wafanyabiashara wengine wakiwamo wanaokuja nchini kununua bidhaa na kuzipeleka nje.

Wito huo umetolewa leo na Seka Kasera, ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Miliki Ubunifu kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), wakati akifungua kongamano la Jumuia ya wafanyabiashara jijini Dar es Salaam.

Katika kongamano hilo alisisitiza kuwa wafanyabiashara wanatakiwa kuwa na elimu ya kutosha kuhusu alama za biashara ili kuhakikisha wanapata mafanikio kupitia shughuli zao na kuinua uchumi wao na nchi kwa ujumla.

"Leo tumekutana na viongozi wa Jumuia za wafanyabishara kupitia jumuia zao wakiwamo wanachama wa STI, TPSF,TCCIA na Jumuia ya Wafanyabiashara Kariakoo ikiwa ni sehemu ya mkakati wetu kuhakikisha tunakutana na kubadilishana mawazo ili kuweka mikakati ya pamoja ili kufikia malengo," amesema.

Aliongeza kuwa ili nchi isonge mbele inahitajika teknolojia ya hali ya juu ya Miliki Bunifu na kwa kuwa  Tanzania ya sasa ni ya viwanda, hivyo wamiliki wa viwanda  wanatakiwa kuuza bidhaa zao kwa kutumia alama zao za biashara.

Alibainisha kuwa wafanyabiashara wengi wanatoa bidhaa nje ya nchi hivyo wanatakiwa kuwa na elimu ya kutosha kuhusu Miliki Bunifu na kuzilinda ili kusaidia kupunguza migogoro ya kugombania alama za biashara.

Aliongeza wafanyabiashara watakapofanikiwa kulinda alama zao za biashara watasaidia kulinda viwanda vya ndani kwa kutoingizwa kwa bidhaa feki ambazo zimekuwa zikiyumbisha uchumi wa nchi.

Pia alibainisha kuwa baada ya kutoa elimu hiyo kwa wafanyabiashara wa Dar es Salaam kupitia vyama vyao, watakwenda mikoani na wataanza na mikoa ya Kanda ya Ziwa na Mbeya ambapo watakutana na jumuia za wafanyabiashara wakubwa na wadogo.

Kasera alibainisha kuwa elimu hiyo itasambazwa nchini kote kupitia wafanyabiasha wadogo na wakubwa ili kutimiza malengo ambayo yamekusudiwa ikiwamo kuongeza thamani ya bidhaa na kuzilinda.

"Lengo ni kuhakikisha wafanyabiashara wanafanya vema katika nyanja za biashara ndani na nje ya nchi ili kuinua uchumi wetu na wanaponunua bidhaa za nje waweze kuzidhibiti vema wanapoziuza kwa wengine," amesema.

Kasera aliweka wazi kuwa mbali na kuendelea kufanya mchakato huo wa kutoa elimu kwa wafanyabiashara pia wanajipanga kushindanisha wanafunzi kuanzia ngazi ya Shule ya Msingi hadi Chuo Kikuu ili kupata wanafunzi wabunifu ambao watasaidiwa kutafutiwa masoko na kuendelezwa.

Kwa upande wake, Martine Mbwana, ambaye ni Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Kariakoo, ambaye ameshiriki mafunzo hayo amesema kuwa Brela kutoa mafunzo hayo ni jambo jema ila akawataka kufika katika maeneo yao ya biashara ili kuzungumza na wafanyabiashara.

"Nashukuru kwa Brela kutukumbuka lakini ni vema wakafika katika maeneo yetu ya biashara ili kutoa elimu hii kwa pamoja ili kila mfanyabiashara imfikie moja kwa moja kupitia maafisa wa Brela," amesema.
MWISHO

Post a Comment

Previous Post Next Post