*Huduma zote za mfuko ni bure
*Wanachama wakipokea simu tata watoe taarifa Polisi
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Mfuko
wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umetoa wito kwa
Wastaafu na Wanachama wote kuwa makini na wimbi la matapeli wanaotoa
taarifa za uongo kwa Wananchama wake kwa lengo la kujipatia kipato kwa
njia zisizo halali.
Kauli
hiyo imetolewa na Afisa Uhusiano Mkuu wa PSSSF, Bw. Abdul Njaidi,katika
Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayoendelea katika viwanja vya
Rocky City Mall jijini Mwanza na kuhudhuriwa na watu mbalimbali kwa
lengo kupata elimu.
Katika maonesho hayo, Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na washiriki mbalimbali huendesha darasa kila siku kwa lengo la kutoa elimu kwa kina juu ya sekta inayotoa elimu kwa siku husika, ambapo Bw. Njaidi alitumia siku ya darasa la Hifadhi ya Jamii kutoa tahadhari juu ya uwepo wa matapeli wanaowalenga Wastaafu na Wanachama wa PSSSF. Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo ni, Elimu ya Fedha kwa Maendeleo ya Watu.
“Kumekuwa na wimbi kubwa la matapeli ambao wanawalenga Wastaafu wetu, kwa kuwarubuni kwa lengo la kujipatia fedha kutoka kwa Wastaafu wetu hao, jambo ambalo sio zuri hata kidogo” alifafanua Bw. Njaidi.
Bw.
Njaidi alisema huduma za PSSSF ni bure na hakuna huduma inayolipiwa na
kuwataka wanachama wanapopigiwa simu za kuwataka kutoa fedha watoe
taarifa Polisi au katika ofisi za PSSSF ambazo zipo kila Mkoa Tanzania,
ikiwemo na ofisi ya Zanzibar.
“Kanda
ya ziwa mnapaswa kuwa makini zaidi, kwani kuna mtuhumiwa mmoja
anayedaiwa kujihusisha na kutapeli Wastaafu ambaye alitiwa mbaroni
jijini hapa” alifafanua Bw. Njaidi
Katika
Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha, watu wanaotembelea katika banda
la PSSSF ambalo lipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu wanajipatia huduma
mbalimbali ikiwemo; elimu juu ya Hifadhi ya Jamii, mafao yatolewayo na
PSSSF, kujihakiki, kuangalia taarifa za michango yao, kufuatilia mafao
yao na kupata taarifa mbalimbali za uwekezaji wa Mfuko.
“Kwa
kweli wanachama wa Mfuko wanajitokeza kupata huduma mbalimbali, mpaka
sasa wengi wanaofika wanahitaji kujua juu ya taarifa zao za michango.
Pia katika banda letu tunatoa elimu ya huduma ya PSSSF kiganjani ambayo
ni njia rahisi kwa wanachama kufuatilia huduma mbalimbali za Mfuko
kupitia simu yake ya kiganjani” alieleza Bw.Njaidi.
PSSSF
imekuwa ikishiriki katika maonesho mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu
kwa umma juu ya huduma na bidhaa zinazotolewa kwa Wanachama na
Watanzania kwa jumla.
Afisa Uhusiano Mkuu wa PSSSF, Bw. Abdul Njaidi akitoa elimu katika semina iliyoandaliwa na Wizara ya Fedha katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayoendelea jijini Mwanza.
Afisa Uhusiano Mkuu wa PSSSF, Bw. Abdul Njaidi akitoa elimu katika semina iliyoandaliwa na Wizara ya Fedha katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayoendelea jijini Mwanza.
Mkurugenzi wa Fedha wa PSSSF, Bi. Beatrice Lupi., akitoa huduma kwa mmoja wa wanachama waliofika katika banda la PSSSF