Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
22/11/2022
Shirika la Children’s Heart Charity Association la nchini Kuwait
linalotoa msaada wa matibabu ya moyo limepanga kuboresha huduma za
kibingwa za matibabu kwa watoto nchini kwa kushirikiana na Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Licha
ya huduma za kibingwa shirika hilo pia limepanga kujenga jengo jipya la
JKCI, kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya wa JKCI, kutoa vifaa tiba na
kuiwezesha Taasisi hiyo kutoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo kwa
wananchi kwa kuwafuata mahali walipo.
Watalaam
wa shirika hilo walitembelea taasisi hiyo leo na kuona watoto
wanaotibiwa JKCI walifarijika kuona uwekezaji mkubwa uliofanywa na
serikali kwa ajili ya matibabu ya moyo yanayotolewa hapa nchini kwa
watanzania wenye uhitaji wa huduma hizo.
Akizungumza
wakati wa ugeni huo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema Shirika la Children’s Heart
Charity Association limeahidi kuangalia kama kutakuwa na uwezekano wa
kujenga jengo jipya la JKCI ambalo litaongeza upatikanaji wa huduma za
matibabu na upasuaji wa moyo hususani kwa watoto.
“Katika
kushirikiana nasi wataalam hawa wameahidi pia kutuletea vifaa tiba
ambavyo vitatumika katika matibabu ya watoto ikiwa ni sehemu ya kutoa
huduma rafiki kwa watoto kwani watoto wengi wanatoka katika familia
zisizokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu,” alisema Dkt. Kisenge.
Dkt.
Kisenge alisema Shirika hilo pia limeahidi kushirikiana na JKCI kutoa
mafunzo kwa wataalam kwa kuwaleta wataalam wao hapa nchini kubadilishana
uzoefu na wataalam JKCI lengo likiwa ni kuifanya taasisi hiyo kuwa bora
nchini Tanzania na Afrika yote.
“Magonjwa
ya moyo kwa watoto yanazidi kuongezeka hapa nchini hivyo kuongeza
uhitaji wa matibabu ya magonjwa hayo kuwa kubwa, naamini ujio wa
wataalam hawa kutoka nchini Kuwait utaenda kusaidia watoto wengi
kufikiwa na matibabu haya ya moyo,” alisema Dkt. Kisenge.
Aidha
Dkt. Kisenge alisema JKCI katika mpango mkakati wake wa kutoa huduma
bora na rafiki kwa watanzania imekuwa ikiwafuata wananchi mahali walipo
ili kila mwenye uhitaji na huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo aweze
kuzipata jambo ambalo limeungwa mkono na watalaam hao kutoka Shirika la
Children’s Heart Charity kwa kuahidi kuiwezesha JKCI ili iweze
kuwafikia wananchi nchi nzima.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Prof. William Mahalu alisema watalam wa afya kutoka
nchini Kuwait wameonesha nia ya kusaidia kutibu watoto wenye magonjwa ya
moyo nia ambayo sio kila mtu anaweza kujitoa kwa ajili ya watoto hao.
“Tumeainisha
mahitaji tuliyonayo ikiwemo ucheleweshwaji wa watoto kufikishwa
hospitali kwa ajili ya matibabu hivyo kuwaomba watusaidie vitendea kazi
ambavyo zitakuwa mikoa yote hapa nchini ili tuweze kutoa huduma za
utambuzi wa magonjwa haya na kuwabaini mapema watoto wenye magonjwa ya
moyo,”.
“Kwa
hapa tulipo sasa tupo katika nafasi nzuri ya kutoa huduma za matibabu
ya moyo kwani zimepunguza matatizo kwa asilimia kubwa lakini bado
tunahitaji kufanikiwa zaidi hivyo tumewaomba wasichoke kubadilishana
nasi uzoefu ili tuweze kupanda zaidi katika kutoa huduma za kibingwa za
matibabu ya moyo,” alisema Prof. Mahalu.
Naye
Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua kwa watoto kutoka
Shirika linalotoa msaada wa matibabu ya moyo kwa watoto la Children’s
Heart Charity Association lililopo nchini Kuwait Faisal Al-Saiedi
alisema Shirika hilo limekuwa likitoa msaada wa matibabu kwa watoto
wengi duniani na sasa likaona ni vizuri kama litawafikia watoto wa
Tanzania ili nao waweze kufaidika na msaada wa matibabu hayo.
“Natambua
kuwa kuna watoto wengi wanaohitaji msaada wa matibabu ya moyo hapa
Tanzania, na wataalam wa hapa wanafanya kazi nzuri kuwasaidia watoto hao
hivyo nasi tunataka kushirikiana nao kuwasaidia watoto hao lakini pia
kuwavusha hatua moja zaidi katika kutoa huduma bora za matibabu ya moyo
kwa watoto wetu,” alisema Dkt. Faisal.
Wataalam
wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakishirikiana na
mwenzao kutoka Shirika linalotoa msaada wa matibabu ya moyo kwa watoto
la Children’s Heart Charity Association lililopo nchini Kuwait Dkt.
Faisal Al-Saiedi kuangalia picha ya tundu lililopo kwenye moyo kwa
kutumia mashine ya Trans esophageal ECHO kwa mtoto ambaye anarudiwa
upasuaji wa moyo wa kuziba tundu na valvu inayovuja walipotembelea JKCI
kwa kuangalia namna ya kushirikiana na Taasisi hiyo leo jijini Dar es
Salaam.
Madaktari
bingwa wa moyo kwa watoto kutoka Shirika linalotoa msaada wa matibabu
ya moyo kwa watoto la Children’s Heart Charity Association lililopo
nchini Kuwait wakiangalia huduma zinazotolewa katika moja ya chumba cha
kliniki ya magonjwa ya moyo kwa watoto walipotembelea JKCI kwa ajili
kuangalia namna ya kushirikiana na Taasisi hiyo leo jijini Dar es
Salaam.
Daktari
bingwa wa Upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Godwin Sharau akiwaelezea aina ya upasuaji wa moyo
wanaoufanya kwa watoto Madaktari bingwa wa moyo kwa watoto kutoka
Shirika linalotoa msaada wa matibabu ya moyo kwa watoto la Children’s
Heart Charity Association lililopo nchini Kuwait walipotembelea Taasisi
hiyo kwa ajili ya kuona namna ya kushirikiana na Taasisi hiyo leo Jijini
Dar es Salaam.
Daktari
bingwa wa usingizi kutoka Shirika linalotoa msaada wa matibabu ya moyo
kwa watoto la Children’s Heart Charity Association lililopo nchini
Kuwait Hesham Menshawy akielezea namna ambavyo shirika hilo
litashirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kutoa huduma za
matibabu ya moyo kwa watoto walipotembelea JKCU leo jijini Dar es
Salaam. Picha na JKCI