Na WAF, DSM
Kuelekea katika Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani Desemba 01, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Ukimwi (UNAIDS) pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo wamezindua Ripoti ya Kidunia ya hali ya Ugonjwa wa Ukimwi kwa Mwaka 2022.
Hafla ya Uzinduzi wa Ripoti hiyo imeongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Utawala Mheshimwia George Simbachawene, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel Mkurugenzi Mtendaji UNAIDS Bi. Winnie Byanyima pamoja na Watendaji wa Taasisi zinazoshughulika na masuala ya UKIMWI.
Ripoti hiyo iliyopewa jina la ‘Dangerous Inequalities’ imebainisha jinsi kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia kunavyopelekea athari katika kufanya maamuzi sahihi kwenye mapambano dhidi ya VVU kwa watoto na watu wazima.
“Hali ya kutokuwa na usawa wa kijinsia ina mchango mkubwa katika maambukizi mapya ya VVU, Vijana wadogo hasa wasichana wako katika hatari mara tatu zaidi kupata maambukizi ya VVU dhidi ya ukilinganisha na vijana wakiume” amebainisha Bi. Winnie Byanyima akiwa anatoa ripoti hiyo.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa toka mwaka 2010 maambukizi ya VVU yamepungua kwa asilimia 62 kwa watu wenye umri wa miaka 15-49 wanaoishi katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, na asilimia 58 kwa Ukanda wa Afrika ya Magharibi.
Kwa upande wa Serikali, akizungumza Waziri Simbachawene amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inathamini mchango mkubwa unaotolewa na Wadau katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi Vya Ukimwi na itaendelea kutoa kipaumbele na kutenga rasilimali katika mapambano zaidi dhidi ya VVU.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema kuwa Serikali imewekeza nguvu nyingi katika kuelimisha Jamii kujikinga dhdi ya maambukizi ya VVU pamoja na kujenga miundombinu ya kutolea huduma, kununua na kusimika mitambo na vifaa tiba vya kisasa na kuajiri wataalam.