TAWOSKA na Wizara wajadili kukuza Karate.

Na John Mapepele

Naibu Katibu Mkuu wa Utamaduni,  Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu amekutana  na viongozi wa chama cha Wanawake wa Karate Tanzania ( TAWOSKA) kujadili jinsi ya kuendeleza  mchezo huo kwa Wanawake hapa nchini.

Aidha, ameipokea  mikakati mbalimbali ya chama hicho na kuwashauri kujipanga vizuri kwa kuwa na mikakati madhubuti itakayosaidia kukuza mchezo huo ili kusambaa nchini kama michezo mingine na kufanya vizuri katika mashindano ya dunia.

Baadhi ya mambo ambayo amekitaka TAWOSKA kufanyia kazi mara moja ni pamoja na kuandaa Mpango Mkakati ambao utakuwa dira ya  utendaji kazi na kuahidi kuwa wizara itasaidia kuwapatia mtaalam wa kuuandaa.

Kuwa na kalenda  ya mwaka ya mchezo huo, kusambaza mchezo huo nchi nzima badala ya sasa ambapo umejikita jjini Dar es Salaam.

Kuanzisha  vilabu vya mchezo wa Karate nchi nzima na ushirikiano na wadau mbalimbali wa ndani ya nchi na mashirikisho ya  kimataifa ya mchezo huo.

Kwa upande wake Mwenyekiti  wa chama hicho, Levina Tarimo  ameishukuru Serikali kwa kutoa kipaumbele kwenye michezo ikiwa ni pamoja na mchezo wa Karate.

Amefafanua kuwa TAWOSKA kimedhamilia kukuza mchezo huo kwa kuendelea kuandaa mashindano mengi zaidi, kutoa mafunzo na kufikia makundi mengi ikiwa ni pamoja na Walemavu.

Amesema wanawake wamekuwa wakifanya vizuri zaidi kwenye mashindano ya kimataifa  na kutoa mfano wa shindano la Afrika lililofanyika nchini Kongo hivi karibuni na wanawake kunyakua medali nyingi.


Post a Comment

Previous Post Next Post