Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), wametakiwa kuzingatia Sheria, kanuni, Muundo na miongozo ya baraza hilo ili kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia utawala bora.
Wito huo umetolewa leo tarehe 12 Novemba, 2022 na
Kamishna Msaidizi kutoka Wizara ya Kazi Bw. Andrew Mwalwisi, alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu Baraza la Wafanyakazi, kama chombo cha kuishauri menejimenti katika utoaji huduma kwa ufanisi.
Bw. Mwalwisi amesema Baraza ni kigezo cha utawala bora kwani uwepo wake kunakuwa na uwajibikaji, utawala wa Sheria pamoja na ushirikishaji katika maamuzi.
Bw. Mwalwisi amesema pia Baraza la Wafanyakazi ni chombo cha mashauriano chenye lengo la kuimarisha mahusiano mema sehemu za kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo.
Amesisitiza kuwa taasisi inapaswa kufanya maaamuzi yote kupitia Baraza la Wafanyakazi kwani ushirikishwaji wa watumishi ni jambo la muhimu.
"Baraza lina wajibu wa kuishauri Menejimenti namna ya kushirikiana na wafanyakazi, kurekebisha mapungufu yaliyopo ikiwa ni pamoja na kushukuru viongozi kwa mambo mazuri waliyofanya," amefafanua Bw. Mwalwisi.
Wakati huohuo Mwenyekiti wa TUGHE mkoa wa Dar es Salaam Bw. Brendan Maro, ameishukuru BRELA kutokana na ushirikiano wa kutosha inaoupata kupitia chama cha Wafanyakazi.
Bw. Maro amesema TUGHE itaendelea kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanachama wake ili watimize wajibu wao kikamilifu pamoja na kutumia fursa ya mafunzo hayo kuitangaza Taasisi.
" Ni wazi kwamba mabadiliko makubwa yametokea kitaasisi ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa haki na maslahi ya watumishi," amefafanua Bw. Maro.
Akifunga kikao cha Baraza hilo Mwenyekiti wa Baraza Bw. Godfrey Nyaisa, ameeleza kuridhishwa kwake na ushiriki wa wajumbe katika kujadili na kuchangia hoja mbalimbali zilizojikita katika kufikia malengo ya Taasisi.
Bw. Nyaisa amewataka wajumbe wa Baraza kufikisha taarifa kwa watumishi wanaowawakilisha juu ya maazimio yaliyofikiwa ikiwa ni pamoja na kuandaa mpango kazi katika maeneo yanayohitaji maboresho.
Kikao cha Baraza kilichoanza jana tarehe 11Novemba, 2022 mkoani Morogoro kimehitimishwa leo tarehe 12 Novemba, 2022 baada ya kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa malengo ya Taasisi kwa mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na kupitia na kuridhia nyaraka mbalimbali za Taasisi.