Na John Mapepele
Rais
Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameipongeza Wizara ya Utamaduni,
Sanaa na Michezo kwa kazi kubwa inayoifanya ambayo imesababisha kuwa
miongoni mwa sekta zinazokuwa kwa kasi na kuchangia kwa kiasi kikubwa
kwenye uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Mhe.
Kikwete ameyasema haya Usiku wa kuamkia leo Novemba 6, 2022 akiwa Mgeni
wa rasmi kwenye uzinduzi wa albamu ya Ommy Dimpoz iitwayo Dedication
mara baada ya kukaribishwa kutoa hotuba yake na Waziri wa Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa ambaye amekuwa mgeni wa
heshima kwenye uzinduzi huo.
Amefafanua
kuwa katika awamu hii ya Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu
Hassan tasnina ya muziki wa kizazi kipya imekua kwa kasi na kupata
mafanikio makubwa ukilinganisha awamu zilizopita.
“Kila
siku nikiangalia kwenye televisheni naona wanamuziki na wasanii wapya
hali ambayo inaashiria kumekuwa na ukuaji wa kasi na kusababisha ajira
kwa vijana” ameongeza Mhe. Kikwete.
Aidha,
amesema changamoto iliyopo kwa sasa kwenye tasnia ya muziki ni namna
gani ya kuhakikisha wanamuziki wanapata malipo kwa kazi zinazopigwa
kwenye vyombo vya Habari na kusisitiza Serikali kupata ufumbuzi wa
kudumu wa suala hili ili kuwasaidia wanamuziki waweze kunufaika na jasho
la kazi zao.
Ametoa
wito kwa Serikali kuendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa haki za
wanamuziki zinalindwa kisheria ili wanamuziki waweze kufanikiwa huku
akifafanua kuwa duniani kote wanamuziki na wasanii wanaongoza kwa kuwa
na vipato vikubwa.
Amempongeza
Mtendaji Mkuu mpya wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Dkt. Kedmon
Mapana kwa kuteuliwa na Mhe. Rais kushika nafasi hiyo huku akimwelezea
kuwa anauwezo na mchango mkubwa kwenye sekta ya Sanaa nchini na kumtaka
kuendelea kutoa mchango huo kwa faida ya taifa la Tanzania.
Kwa
upande wake, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed
Mchengerwa wakati akimkaribisha Rais mstaafu Kikwete ili aweze kutoa
hotuba yake amesema Sekta ya Sanaa ndiyo sekta iliyoongoza kwa kasi
ya ukuaji na kufafanua kuwa mwaka uliopita iliongoza kwa kukua ambapo
ilikuwa kwa 19% na kwamba dhamira ya Serikali ni kutaka sekta hiyo
kuendelea kukua kwa kasi ili iweze kuchangia kwenye uchumi wa nchi
na kutoa ajira za uhakika kwa vijana.
Aidha
amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu
Hassan kwa maono yake makubwa na msukumo anaoutoa kwenye sekta hizo
ambao umesaidia kuleta mafaniklio makubwa katika kipindi kifupi cha
utawala wake, huku pia akimpongeza Mhe. Kikwete kwa kazi aliyoifanya ya
kusaidia wasanii katika awamu yake.
“Mhe.
Rais Mstaafu nina furaha ya kueleza kuwa sekta hizi ni sekta za kuleta
furaha kwa wananchi na kwa kweli changamoto kwa sasa tunayoipata
tunaweza kusema ni suala la kuongeza muda wa furaha, tungependa
kuongeza muda wa furaha hasa kwenye majiji hapa nchini ili wananchi
waendelee kufurahi” ameongeza Mhe. Mchengerwa