SERIKALI : TAMASHA LA BAGAMOYO KUWA KUBWA ZAIDI

 



   

****************

Serikali imesema imedhamiria kulifanya Tamasha la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo ambalo ni Tamasha kubwa na kongwe nchini kuwa kubwa zaidi na lenye kuakisi neno “kimataifa.”

Akizungumza na Kamati ya kuratibu maandalizi ya Tamasha hilo iliyoteuliwa hivi karibuni na Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Mohammed Mchengerwa, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi, aliyekutana na Kamati hiyo leo mjini Bagamoyo amesema, Kamati imeaminiwa na imepewa jukumu zito hivyo wajipange kutekeleza jukumu hilo ili kufanya mageuzi makubwa na ya haraka.

“Kupitia Tamasha hili ni mikakati ya Serikali kuiweka Tanzania kimataifa zaidi hivyo tunataka tufikie viwango vya juu kwa kuwa ubunifu hauna ukomo wala hauna mwisho,” amesema Dkt. Abbasi.

Naye Mkuu wa Wilaya mwenyeji wa Tamasha hilo la Bagamoyo Mhe. Zainab Abdallah amesema Wanabagamoyo wako tayari kushirikiana na Kamati hiyo kwani wao ndio wanufaika wakubwa kiuchumi na kijamii.

Awali wakati wa ukaribisho Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Herbert Makoye ameishukuru Serikali kwa jitihada kubwa inazozifanya kupitia Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo katika kuhakikisha Tamasha la Bagamoyo linakua bora zaidi na la viwango vya Kimataifa.

Post a Comment

Previous Post Next Post