RAIS SAMIA ATOA WITO KWA VIONGOZI WA NCHI ZA AFRIKA KUUNGANA VITA DHIDI YA BIASHARA HARAMU YA MAZAO YA MISITU

 Na Sixmund Begashe NMRT


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa viongozi Wakuu wa nchi za Afrika wachukue hatua za makusudi katika udhibiti wa uvunaji na biashara haramu ya usafirishaji wa mazao ya misitu.

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa wito huo kupitia Hotuba iliyosomwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Kikanda wa Usimamizi Endelevu wa Misitu ya Miombo uliofanyika jijini Maputo Msumbiji.

Kupitia hotuba hiyo Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi jirani, Taasisi na Mashirika mbalimbali katika kupiga vita uvunaji haramu na biashara haramu ya mazao ya misitu na kuweka msisitizo mkubwa katika uhifadhi Misitu ya Miombo ili kulinda Ikolojia na fukwe za Bahari kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

“ Wote lazima tuungane katika kukabiliana na tatizo hili la uvunaji mkubwa wa misitu usio endelevu ambao umekua tishio kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kilimo,uchomaji wa misitu, kushindwa kwa sera na masoko yetu, utegemezi wa muda mrefu wa matumizi ya kuni kama nishati, matumizi kupita kiasi ya rasilimali misitu na kukosekana kwa mipango bora ya matumizi ya ardhi. Sote tukiungana kwa pamoja tutazishinda changamoto hizi” Amesisitiza.

Ameeleza kuwa chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Tanzania imetoa kipaumbele kikubwa katika Uhifadhi wa Misitu na ikolojia yake kwa kuwashirikisha wananchi kwenye maeneo yao kuhifadhi na kulinda rasilimali za misitu zinazowazunguka na kuongeza kuwa uhifadhi wa Misitu ya Miombo Barani Afrika una umuhimu mkubwa katika kulinda fukwe za bahari na viumbe waishio baharini pamoja na shughuli za utalii.

Mkutano huo wa Kimataifa wa Kikanda wa Usimamizi Endelevu wa Misitu ya Miombo umehudhuriwa na Rais wa Msumbiji Mhe. Filipe Jacinto Nyusi, Rais wa Zimbabwe Mhe. Emmerson Mnangagwa, Mabalozi kutoka nchi mbalimbali, viongozi wa Serikali na Mashirika ya Kimataifa.

Post a Comment

Previous Post Next Post