TAARIFA YA KAMATI YA SERA YA FEDHA YA BENKI KUU YA TANZANIA (MPC)


 Kamati imeridhishwa na utekelezaji wa sera ya fedha, uliopelekea kuwepo ukwasi wa kutosha katika  mabenki, na hivyo kuchochea ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi. Hata hivyo, Kamati imeendelea kufuatilia  kwa karibu ongezeko la mfumuko wa bei kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, hali ambayo inaweza kuathiri kasi ya ukuaji wa uchumi nchini. 

Uchumi wa dunia umeendelea kukabiliwa na athari za vita nchini Ukraine, kuibuka upya kwa maambukizi  ya UVIKO-19 nchini China, ongezeko la mfumuko wa bei, pamoja na mazingira magumu ya kifedha katika  soko la dunia. Athari hizi zimeendelea kudumaza kasi ya kuimarika kwa uchumi wa dunia na hivyo  kupelekea Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kushusha makadirio ya ukuaji wa uchumi wa dunia kwa  mwaka 2022 na 2023, ikilinganishwa na makadirio ya awali. 

Mwenendo wa hali ya uchumi katika nusu ya kwanza ya mwaka 2022, umebakia sambamba na makadirio ya  ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2022 wa asilimia 4.7 na asilimia 5.4 kwa Tanzania Bara na Zanzibar, mtawalia.  Mfumuko wa bei uliongezeka kufikia asilimia 4.0 na asilimia 4.4 mwezi Mei na Juni 2022, mtawalia, kutokana  na kupanda kwa bei za bidhaa kutoka nje ya nchi, japo umebaki ndani ya lengo la asilimia 3-5 kwa Tanzania  Bara na asilimia 5 kwa Zanzibar. Aidha, kasi kubwa ya kuendelea kuongezeka kwa bei za chakula, nishati na  mbolea katika soko la dunia, zinaashiria uwezekano wa ongezeko la mfumuko wa bei nchini kwa siku za usoni. 

Ujazi wa fedha umeendelea kuongezeka sanjari na lengo la ukuaji kwa mwaka 2021/22, ikiwa ni matokeo ya  utekelezaji wa sera wezeshi ya fedha na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi nchini. Ukuaji wa mikopo kwa  sekta binafsi pia umeongezeka kwa kasi ya kuridhisha na kufikia wastani wa asilimia 9.9, sanjari na lengo la  mwaka 2021/22. Utekelezaji wa sera ya bajeti kwa mwaka 2021/22 ulikuwa wa kuridhisha, huku viwango vya  ukusanyaji wa mapato vikiendelea kuongezeka. Sekta ya nje imeendelea kukabiliwa na changamoto za  ongezeko la bei za bidhaa katika soko la dunia, na athari za Benki Kuu katika nchi mbalimbali duniani kuanza  utekelezaji wa sera ya fedha yenye kupunguza ukwasi ili kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei. Hata hivyo, akiba  ya fedha za kigeni imeendelea kubakia katika viwango vya kuridhisha, kutosheleza mahitaji ya uagizaji wa  bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi kisichopungua miezi 4.6 mwezi Juni 2022. Mwenendo huu  umeendelea kuchangia utulivu wa thamani ya shilingi nchini. 

Kwa kuzingatia tathmini ya mwenendo wa uchumi wa Tanzania na dunia, Kamati ya Sera ya Fedha,  imeridhia Benki Kuu ya Tanzania kupunguza kasi ya kuongeza ukwasi kwenye uchumi katika nusu ya pili  ya mwaka 2022, ili kukabiliana na athari za ongezeko la mfumuko wa bei, bila kuathiri kasi ya ukuaji wa  uchumi. Aidha, Kamati imesisitiza umuhimu wa Benki Kuu ya Tanzania kuendelea kuwa na akiba ya  kutosha ya fedha za kigeni, ili kuendelea kudumisha utulivu wa thamani ya shilingi na kulinda uchumi dhidi  ya athari za kuongezeka kwa bei za bidhaa katika soko la dunia. 

Gavana 

Benki Kuu ya Tanzania 

Post a Comment

Previous Post Next Post