BENKI KUU YATAKIWA KUONGEZA UFADHILI WA WANAFUNZI VYUO VIKUU

 

 Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Hussein Kattanga (kushoto) akielezea jambo kwa Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Yamungu Kayandabila, alipotembelea banda la BoT katika Maonesho ya Nanenane Mbeya. 

Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Hussein Kattanga (katikati) akizungumza na Mkurugenzi wa Utumishi na Uendeshaji BoT, Bw. Kened Nyoni, kuhusu kurugenzi hio alipotembelea banda la BoT katika Maonesho ya Nanenane Mbeya. Kulia ni Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Yamungu Kayandabila na Kaimu Meneja Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki, Bi. Victoria Msina. 

Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Hussein Kattanga, akizungumza na Mkurugenzi wa Bodi ya Bima ya Amana, Bw. Isack Kihwili kuhusu namna Bodi inavyokinga amana za wateja katika mabenki. Wapili kutoka kushoto ni Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Yamungu Kayandabila na Afisa Mwandamizi wa Bodi, Bi. Joyce Shala.  

Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Hussein Kattanga, akioneshwa alama za usalama katika noti zetu na Meneja Idara ya Sarafu BoT, Bw. Ilulu Ilulu, alipotembelea banda la BoT katika Maonesho ya Nanenane Mbeya. Wa pili kutoka kulia ni Kaimu Meneja Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki, Bi. Victoria Msina.  

Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Hussein Kattanga, akizungumza na Afisa Mkuu Mwandamizi kutoka Kurugenzi ya Mifumo ya Malipo ya Taifa , Bi. Joyce Njau, kuhusu namna BoT inasimamia mifumo ya malipo nchini. Kutokea kulia ni Mkurugenzi Tawi la BoT Mbeya, Bw. Ibrahim Malogoi, Naibu Gavana BoT, Dkt. Yamungu Kayandabila, Kaimu Meneja Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki, Bi. Victoria Msina na Afisa Mkuu Mwandamizi wa Uhusiano wa Umma, Bw. Lwaga Mwambande.  

Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Hussein Kattanga akipewa maelezo na Mratibu wa Mafunzo ya Muda Mfupi kutoka Chuo cha BoT, Bi. Tulla Mwigune, alipotembelea banda la BoT kwenye Maonesho ya Nanenane Mbeya. Kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Utumishi na Uendeshaji BoT, Bw. Kened Nyoni, Meneja Idara ya Sarafu BoT, Bw. Ilulu Ilulu, Naibu Gavana BoT, Dkt. Yamungu Kayandabila, Afisa Uhusiano wa Umma na Itifaki BoT, Bi. Beatrice Ollotu na Kaimu Meneja Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki, Bi. Victoria Msina (kushoto)

************************

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein Katanga ameitaka Benki Kuu ya Tanzania kuongeza idadi ya wanafunzi inayowadhamini kwa masomo ya elimu ya juu kuliko, akisema idadi ya wanafunzi inaowadhamini sasa bado ni ndogo sana.

Alisema hivyo tarehe 7 Agosti 2022 wakati alipotembelea banda la Benki Kuu ya Tanzania katika Maonesho ya Nanenane kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

“Kwanini msiongeze idadi ya wanafunzi mnaowapatia udhamini kwa mwaka? Uchumi unabadilika na mahitaji yanaongezeka. Fikiria kudhamini wanafunzi 100 wa kike na 50 wa kiume kwa mwaka,” alishauri Katibu Mkuu Kiongozi.

Aidha, Katibu Mkuu Kiongozi alitaka udhamini huo usiishie katika masomo ya uzamili, bali uendelee hadi kufikia uzamivu ili kuendana na mahitaji ya ulimwengu wa sasa.

Mapema Mkurugenzi wa Utumishi na Uendeshaji wa Benki Kuu, Bw. Kened Nyoni, alimweleza kwamba hadi hivi sasa (tangu 2013/14) Benki Kuu imetoa udhamini wa shahada ya kwanza na ya uzamili kwa wananfunzi 61 kupitia Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere. Aidha zaidi ya wanafunzi 30, wamenufaika na udhamini wa shahada ya uzamili ya uchumi kupitia Mfuko wa Kumbukumbu ya Gilman Rutihinda.

Bw. Nyoni alimweleza Katibu Mkuu Kiongozi kwamba kupitia Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius K. Nyerere Benki Kuu ilikuwa inatoa udhamini kwa wanafunzi watano kwa mwaka na sasa imeongeza idadi hiyo hadi kufikia wanafunzi 10 kwa mwaka, idadi ambayo Katibu Mkuu Kiongozi alisema bado ni ndogo sana.

Aidha, Balozi Katanga, ambaye alikaribishwa katika banda la BoT na Naibu Gavana, Dkt. Yamungu Kayandabila na viongozi wengine, ametoa wito kwa taasisi za kuendeleza ujuzi wa wafanyakazi kuhakikisha hazitoki katika wajibu huo na kuanza kufundisha taaluma.

Alisema hayo wakati alipopata maelezo kuhusu shughuli za Chuo cha BoT kilichoko Mwanza. Balozi Katanga alisema vyuo vingi ambavyo vililenga kujenga uwezo kwa wafanyakazi ili kuendana na kazi zao, vimejikuta vinafundisha taaluma zaidi badala ya kuongeza ujuzi wa stadi za kazi kwa wafanyakazi.

Katibu Mkuu Kiongozi alikitaka Chuo cha Benki Kuu ambacho kinatarajia kuanza kutoa wahitimu wa kwanza wa Diploma mwezi Novemba mwaka huu kutathmini endapo malengo yake ya kujenga kizazi cha wafanyakazi wapya wa sekta ya benki yanafanikiwa, bila kuathiri jukumu la kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi waliopo katika sekta hiyo.

“Ng’ang’ana kutoa mafunzo ya kujenga uwezo wa stadi za kazi kwa wafanyakazi badala ya kufundisha taaluma. Benki nyingi zina matatizo mengi ya uaminifu na kuongezeka kwa mikopo chechefu. Msifundishe taaluma na kuacha kujenga uwezo wa stadi za kazi,” aliagiza Balozi Katanga.

Awali, Mratibu wa Mafunzo ya Muda Mfupi katika Chuo cha BoT, Bi. Tulla Mwigune, alimweleza Katibu Kiongozi kwamba chuo hicho hutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu yanayolenga kujenga uwezo wa wafanyakazi katika sekta ya benki.

Alieleza kwamba kuanzishwa kwa mafunzo ya muda mrefu kama Diploma ya Masuala ya Usimamizi wa Benki kunalenga kuwaandaa vijana kuingia katika sekta ya benki, hasa hivi sasa kutokana na kukua kwa sekta ya huduma ndogo za fedha na mahitaji ya watu wenye ujuzi na masuala ya kibenki.

Kuhusu usimamizi wa sekta ya fedha, Katibu Mkuu Kiongozi aliitaka Benki Kuu kuongeza jitihada za usimamizi wa sekta hiyo kwa lengo la kupunguza mikopo chechefu, ambayo inachangia riba kubwa kwa wakopaji. Katika maelezo yake, Mkaguzi wa Mabenki, Bw. Gwamaka Charles, alisema kwa sasa BoT inazitaka benki na taasisi za fedha kuhakikisha zimepitia taarifa za ukopaji za wateja wao kabla ya kuamua kuwakopesha.

Pia, Katibu Mkuu Kiongozi ameitaka Bodi ya Bima ya Amana kuharakisha kupitia kiwango cha juu cha fidia endapo benki inaanguka au kufutiwa leseni badala ya kiwango cha juu cha sasa cha shilingi milioni 1.5. Alisema hivyo baada ya kupata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Bodi ya Bima ya Amana, Bw. Isack Kihwili, kuhusu kazi za bodi hiyo, ambazo ni pamoja na kukinga amana za wananchi zilizoko katika benki na taasisi za fedha zinazosimamiwa na Benki Kuu.

Kuhusu huduma za kibenki, Balozi Katanga ameitaka Benki Kuu kutumia changamoto zinazojitokeza katika masuala ya huduma za kibenki, yakiwemo masuala ya uchakataji wa sarafu, yatumike kuziba mianya yote inayoweza kujitokeza.

Aidha, ameitaka Benki Kuu kuimarisha elimu kuhusu historia ya noti na sarafu kwa ajili ya kuondoa fikira potofu kuhusu matoleo mbalimbali ya noti na sarafu miongoni mwa wananchi. Alisema hivyo baada ya kupata maelezo kutoka Meneja wa Sarafu wa BoT, Bw. Ilulu S. Ilulu kuhusu kazi za Kurugenzi ya Huduma za Kibenki.

Katika maonesho ya mwaka huu ya Nanenane yenye kauli mbiu ya; ‘Ajenda 10/30: Kilimo ni Biashara, Shiriki Kuhesabiwa kwa Mipango Bora ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi’ BoT inatoa elimu kwa wananchi kuhusu kazi zake na jinsi zinavyochangia maendeleo ya kilimo, mifugo na uvuvi, pamoja na kuwahimiza wananchi kujitokeza kuhesabiwa siku ya Sensa ya Watu na Makazi tarehe 23 Agosti mwaka huu.

Maonesho ya Nanenane kitaifa yanatarajiwa kufungwa rasmi tarehe 8 Agosti na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.


Post a Comment

Previous Post Next Post